TAKWIMU KUWA MSINGI WA LENGO LA MAJI KAYA ASILIMIA 90
Nov 19, 2026
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALI imeeleza kuwa upatikanaji wa takwimu sahihi na za uhakika ni miongoni mwa nguzo zitakazosaidia kufanikisha lengo la kuhakikisha angalau asilimia 90 ya kaya nchini zinapata huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2030.
Takwimu hizo zinatarajiwa kusaidia kupima hali ya upatikanaji wa huduma za maji, kubaini maeneo yenye upungufu na kuelekeza uwekezaji kulingana na mahitaji halisi ya wananchi.
Akizungumza katika maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Takwimu Afrika yaliyofanyika jijini Dodoma , Mwenyekiti wa Bodi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Anna Makinda, alisema takwimu rasmi ni nyenzo muhimu katika kupima utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuwezesha watunga sera kufanya maamuzi yanayotokana na ushahidi.
Amesema kufikiwa kwa lengo la kuongeza kaya zinazopata maji safi na salama kunahitaji mifumo imara ya ukusanyaji na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.
"Lengo la kuongeza kaya zinazopata huduma ya maji safi na salama hadi kufikia angalau asilimia 90 ifikapo mwaka 2030 linahitaji takwimu sahihi zinazopatikana kwa wakati ili kupima hatua zinazofikiwa," amesema Makinda.
Amesema pamoja na kuzalisha takwimu, ni muhimu kuhakikisha zinawafikia watumiaji wa mwisho, hususan watunga sera, ili zitumike katika kupanga na kusimamia shughuli za maendeleo badala ya kubaki kwenye nyaraka za ofisi.
"Watunga sera wanapaswa kuhakikisha kuwa takwimu zote zinazopatikana zinawafikia walaji wa mwisho na siyo kuendelea kubaki kwenye makabrasha," amesema.
Makinda alisema Bodi itaendelea kuisimamia menejimenti ya NBS ili kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuzalisha takwimu zinazokidhi mahitaji ya watumiaji.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Ally Munde, alisema matumizi ya takwimu sahihi yana mchango mkubwa katika kuboresha mipango ya maendeleo kwa kusaidia Serikali kutambua mahitaji ya wananchi na kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Amesema taarifa hizo zinapaswa kutumika katika kupanga na kutekeleza miradi ili kuhakikisha uwekezaji unaofanyika unakuwa na tija na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
"Takwimu sahihi ni nyenzo muhimu katika kupanga huduma za kijamii na kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kuhakikisha mipango ya maendeleo inazingatia hali halisi ya wananchi," amesema Munde.
Amesema kaulimbiu ya mwaka huu inayohusu kuimarisha mifumo rasmi ya takwimu za maji na usafi wa mazingira kwa maendeleo endelevu yanayohimili mabadiliko ya tabianchi inapaswa kupewa kipaumbele katika uzalishaji na matumizi ya takwimu nchini.
Amefafanua kuwa takwimu hizo zitasaidia kubaini maeneo yenye changamoto ya huduma za maji na usafi wa mazingira na kuwezesha Serikali kuweka mikakati ya kuboresha huduma hizo.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa takwimu kwa wakati ni muhimu katika kuandaa mipango inayozingatia athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha rasilimali zinazowekezwa zinatumika kwa ufanisi.
Munde amesisitiza kuwa matumizi ya takwimu katika maamuzi ya maendeleo yanapaswa kupewa umuhimu ili kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji unaofanyika katika sekta mbalimbali.



