Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 SEKTA BINAFSI YATAKIWA KUWEKEZA KATIKA MAGHALA YA KISASA

SEKTA BINAFSI YATAKIWA KUWEKEZA KATIKA MAGHALA YA KISASA

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media, Dodoma

SEKTA binafsi imetakiwa kuongeza uwekezaji katika maghala ya kisasa, mitambo ya kukausha na kusindika nafaka pamoja na mifumo ya kidijitali ili kuongeza thamani ya mazao hayo na kuiwezesha Tanzania kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani badala ya malighafi.

Wito huo umetolewa leo Novemba 19, 2026, na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Sempeo Manongi, aliyemwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara katika uzinduzi wa Taasisi ya TanGrainHub uliofanyika jijini Dodoma.

Manongi amesema uwekezaji huo ni muhimu katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya nafaka, kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania na kuhakikisha wakulima pamoja na wafanyabiashara wananufaika zaidi na shughuli za uzalishaji na biashara.

Amesema nafaka ni nguzo muhimu katika usalama wa chakula, ajira, kipato cha wakulima na maendeleo ya viwanda, hivyo mafanikio ya uzalishaji yanapaswa kuambatana na uwepo wa masoko ya uhakika, miundombinu bora ya kuhifadhi na uwezo wa kusindika mazao.

Amesema kiwango cha taifa cha kujitosheleza kwa chakula kwa mwaka wa kilimo 2025/2026 kimezidi asilimia 130, lakini mafanikio hayo yanapaswa kwenda sambamba na uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani.

"Nia ya Serikali ni kuhamasisha uchumi kutoka kuuza nafaka ghafi kwenda kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani, zikiwemo vyakula vilivyosindikwa na chakula cha mifugo vinavyokidhi viwango vya soko," amesema.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kurahisisha taratibu za usajili na utoaji wa leseni, kupanua upatikanaji wa taarifa za masoko na kuimarisha mifumo ya viwango na vipimo.

Aidha, amewataka wazalishaji na wasindikaji kutumia nembo ya taifa ya Made in Tanzania ili kutambulisha bidhaa zinazozalishwa nchini na kuongeza ushindani wake katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema Tanzania ina fursa za kuuza bidhaa zake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), lakini kunahitajika uzalishaji wa bidhaa zenye ubora, kiasi cha kutosha na upatikanaji endelevu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TanGrainHub amesema taasisi hiyo imeanzishwa kuwa jukwaa la kuunganisha wafanyabiashara, wakulima na wasindikaji badala ya kushindana na taasisi nyingine zilizopo katika sekta hiyo.

Amesema itakuwa daraja kati ya wazalishaji, wafanyabiashara, wasindikaji na masoko kwa kuwawezesha kupata taarifa za bei, fursa za biashara, teknolojia, mitaji na huduma nyingine zitakazoongeza ufanisi wa shughuli zao.

Amesema mafanikio ya taasisi hiyo yatategemea ushirikiano wa wadau na utayari wao wa kuitumia katika kukuza biashara za nafaka.

"Kwa pamoja tunaweza kujenga biashara imara, kuongeza thamani ya mazao yetu, kukuza viwanda, kutengeneza ajira na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi yetu Tanzania," amesema.

Ameongeza kuwa taasisi hiyo itashirikiana na Serikali, vyuo vikuu, taasisi za fedha na washirika wa maendeleo katika kutoa maarifa, teknolojia na mitaji kwa ajili ya kuboresha sekta ya nafaka.

Naye mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Upendo Lema, amewataka wafanyabiashara na wasindikaji kuzingatia ubora wa bidhaa zao ili ziweze kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3