KUHARIBU NOTI FAINI YA SH. 500,000 KWA KILA NOTI AU JELA MWAKA MMOJA
Nov 6, 2026
Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio Daima Media
KITENDO cha kuchana, kuchoma au kuharibu noti za fedha kwa makusudi kinaweza kumwingiza mtu Katika mkono wa Sheria huku adhabu yake ikitajwa kuwa faini ya Shilingi 500,000 kwa kila noti au kifungo cha mwaka mmoja jela, kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Masharti hayo yanatajwa katika Kifungu cha 332A cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, kinachohusu uharibifu wa noti na sarafu zinazotambulika kisheria kuwa fedha halali.
Akifafanua Sheria hiyo Afisa wa Benki Kuu , Kurugenzi ya Sarafu, Shadrack Mapunda katika semina ya waandishi wa habari, alisema sheria hiyo inalenga kuhakikisha fedha zinazotumika nchini zinalindwa dhidi ya vitendo vya uharibifu vinavyofanywa bila kufuata taratibu zilizowekwa.
Alisisitiza kuwa ulinzi wa fedha ni sehemu muhimu ya kuimarisha uaminifu katika mfumo wa fedha na kuhakikisha noti zinaendelea kutumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Sambamba na hilo, sheria imeweka pia masharti dhidi ya vitendo vya kughushi fedha na nyaraka mbalimbali. Kifungu cha 338 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kinatajwa kuweka adhabu kali kwa makosa ya kughushi, ikiwemo kifungo cha maisha jela kwa mujibu wa masharti husika.
Aidha, mahakama inaweza kuamuru mali au nyaraka zinazohusishwa na uhalifu huo kutaifishwa kwa mujibu wa sheria.
Hatua hiyo inasisitiza umuhimu wa wananchi kuheshimu fedha za taifa na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha uhalali na uaminifu wa mfumo wa fedha nchini.
...

