VIJANA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UFUGAJI WA SAMAKI KWA VIZIMBA.
Oct 25, 2026
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Vijana nchini wametakiwa kuendelea kuchangamkia fursa za ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ili kujikwamua kiuchumi na kupunguza malalamiko ya ukosefu wa ajira.
Wito huo umetolewa leo, Jumapili, Oktoba 25, 2026, na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Kedmon Mapana, akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, katika hafla ya uvunaji wa samaki waliofugwa kwa njia ya vizimba na kikundi cha Kitwima Youth Group baada ya kuwezeshwa kupitia Programu ya Bilioni 200.
Dkt. Mapana amesema ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ni miongoni mwa fursa zinazoweza kuwasaidia vijana kujiajiri, kujipatia kipato na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali badala ya kutegemea ajira rasmi pekee.
Aidha, amewahimiza vijana kujisajili katika mfumo wa Vijana YES (Youth Empowerment System) ili waweze kutambulika na kuwezesha Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kufahamu mahitaji na vipaumbele vyao katika kila mkoa na kupanga namna bora ya kuwawezesha.
Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi cha Kitwima Youth Group, Bung'e Nawe Kwaangw, amesema kikundi hicho kilipewa kiasi cha Shilingi milioni 106,963,500 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Amesema uwezeshaji huo umekipa kikundi nafasi ya kutekeleza mradi huo kwa lengo la kukuza shughuli za kiuchumi na kuongeza kipato kupitia ufugaji wa samaki.
Naye, baadhi ya wananchi wameeleza namna mradi huo unavyowanufaisha, hususani katika kuwawezesha kupata kipato kupitia shughuli zinazohusiana na ufugaji na uvunaji wa samaki.
Wamesema miradi ya aina hiyo ni muhimu katika kukuza uchumi wa wananchi na kufungua fursa zaidi za kujipatia kipato, huku vijana wakihimizwa kutumia vyema fursa zinazotolewa na Serikali kujiletea maendeleo.

