Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA YATEMBELEA TATC–NYUMBU

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA YATEMBELEA TATC–NYUMBU


Na Matukio Daima Media 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), tarehe 24 Oktoba , 2026, imefanya ziara ya kikazi katika Shirika la Tanzania Automotive Technology Centre (TATC–Nyumbu), lililopo Kibaha, mkoani Pwani, kwa lengo la kufahamu utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo, mafanikio yaliyofikiwa pamoja na changamoto zinazolikabili.

TATC–Nyumbu ni shirika la kimkakati lililo chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, linalojishughulisha na utafiti, uhaulishaji wa teknolojia, uundaji wa vipuri vya magari na utengenezaji wa mitambo. Shirika hilo lina mchango muhimu katika kukuza uwezo wa ndani wa kiteknolojia na kuendeleza sekta ya viwanda nchini.

Kamati hiyo iliongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Paschal Inyasi (Mb), na kupokelewa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho.

 Viongozi wengine waliohudhuria mapokezi hayo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Salum Haji Othman, Mwenyekiti wa Bodi ya TATC–Nyumbu, Balozi na Luteni Jenerali Mstaafu Paul Meela, pamoja na viongozi wengine wa Wizara na Shirika la Nyumbu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho, aliishukuru Kamati ya NUU kwa kutembelea mashirika yaliyo chini ya Wizara hiyo, likiwemo TATC–Nyumbu.

Ameeleza kuwa ziara hiyo ni muhimu kwa kuwa itaiwezesha Kamati kupata uelewa wa kina kuhusu majukumu ya msingi ya shirika, shughuli zinazotekelezwa, mafanikio yaliyopatikana na changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele.

 Aidha, ziara hiyo inatoa fursa ya kuimarisha uelewa na ushirikiano katika kusimamia maendeleo ya mashirika ya kimkakati kwa manufaa ya Taifa.

Kwa upande wake, akitoa majumuisho ya ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya NUU, Mheshimiwa Paschal Inyasi (Mb), amelipongeza Shirika la TATC–Nyumbu kwa juhudi na ubunifu unaoendelea kuoneshwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Amesisitiza kuwa Kamati ina imani kubwa na Shirika hilo, akibainisha kuwa lina mchango muhimu katika kufanya utafiti, kuhamisha teknolojia na kukuza uwezo wa viwanda nchini.

 Ameeleza kuwa shughuli zinazotekelezwa na TATC–Nyumbu ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa Taifa wa kubuni, kuendeleza na kutumia teknolojia zinazochochea maendeleo ya viwanda.

Aidha, Mheshimiwa Inyasi ameeleza kufurahishwa na ziara hiyo na kuipongeza Serikali kwa juhudi zake za kusimamia mashirika ya kimkakati, yakiwemo TATC–Nyumbu, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuyaimarisha ili yaweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Kamati ya NUU za kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na mchango wa taasisi hizo katika kulinda na kuendeleza maslahi ya Taifa.



 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3