SINGIDA YAUNGANA KUFANYA DUA YA MAREHEMU HAFIDH AMEIR
Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
WAUMINI wa dini mbalimbali na viongozi wa chama na serikali mkoa wa Singida wakiongozwa na Kaimu Shehe wa Mkoa wa Singida,Shekhe Issa Simba,wamefanya dua ya kumrehemu aliyekuwa mume wa Rais, marehemu Hafidh Ameir aliyefariki Septemba 7, mwaka huu.
Kaimu Shehe wa Mkoa wa Singida, Shekhe Issa Simba, akizungumza leo (Oktoba 10, 2026) wakati wa dua hiyo ,ameitaka Serikali kuimarisha maendeleo ya mkoa huo kwa kuweka miundombinu muhimu ikiwamo maji safi na salama, reli ya kisasa (SGR), uwanja wa ndege na viwanda vingi ili kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema viongozi wa dini mkoani humo wanaendelea kuhimiza umoja, uzalendo na maendeleo, akisisitiza kuwa mshikamano baina ya wananchi, viongozi wa dini, chama na Serikali ni msingi muhimu wa kufanikisha maendeleo ya mkoa huo.
Amesema viongozi wa dini wamekuwa wakihimiza uzalendo kwa wananchi, ikiwamo kutembelea madarasa ili kuwafundisha vijana umuhimu wa kuipenda nchi yao na dini zao, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuwajenga vijana katika misingi ya amani, umoja na uwajibikaji.
“Viongozi wa dini wa Singida tunatamani kuwa na maendeleo zaidi. Tunahitaji maji bora, SGR, uwanja wa ndege na viwanda vingi ili Wanasingida waweze kunukia kama ilivyo Dodoma,” amesema Shekhe Simba.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kudumisha umoja na kupendana, huku akiwaomba viongozi wa chama na Serikali kuendeleza misingi ya mshikamano iliyojengwa. Pia amewaomba waumini kumuombea Rais Samia ili Mwenyezi Mungu ampe subira na uvumilivu katika kipindi cha majonzi ya kumpoteza mume wake.
Kuhusu mvua za El Niño, Shekhe Simba alisema Mufti Mkuu wa Tanzania amewaelekeza waumini kufunga na kumuomba Mwenyezi Mungu ili mvua hizo zisinyeshe kwa kiwango kitakachosababisha madhara kwa wananchi na mali zao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema wamekutana kumuombea na kumfariji Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha majonzi, huku akiwashukuru wananchi walioshiriki dua hiyo.
Dendego amesema ushiriki wa wananchi katika dua hiyo ni ishara ya mshikamano na upendo, akieleza kuwa sala na salamu zao zitampa Rais nguvu ya kuendelea na majukumu yake. Amewaomba Wanasingida kuendelea kupendana na kumuombea marehemu Hafidh Ameir apumzike kwa amani.
Vilevile, amewataka wazazi na walezi kuwaangalia watoto kwa karibu wakati wa mvua, akisisitiza kuwa hawapaswi kuruhusiwa kucheza kwenye madimbwi ya maji ili kuepusha ajali na madhara yanayoweza kujitokeza.




