NFRA SONGEA YAHIFADHI TANI 150,000 ZA MAHINDI KUKABILIANA NA JANGA LA EL NINO
Oct 29, 2026
Na Thobias Mwanakatwe, SONGEA
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya Songea, umesema umehifadhi zaidi ya tani 150,000 za mahindi, ikiwa ni sehemu ya kiasi cha mahindi kilichotengwa kwa ajili ya kusaidia nchi kukidhi mahitaji ya chakula iwapo nchi itakabiliwa na changamoto ya upungufu wa chakula kutokana na athari za mvua za El Nino.
Hata hivyo, wakala huo umesema unaendelea na ununuzi wa mahindi kwa msimu wa mwaka wa fedha 2026/2027, huku ukikabiliwa na changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara wa kati kushikilia kiasi kikubwa cha mahindi wakisubiri bei ipande zaidi ili wapate faida kubwa.
Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Bw. Zenobius Kahere, akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea kuhusu hali ya ununuzi wa mahindi, alieleza kuwa kanda hiyo imepangiwa kununua tani 235,000 katika mwaka wa fedha 2026/2027.
“Ninaamini bado NFRA itafikia lengo la kununua tani 235,000 katika kipindi kilichobaki. Tunaendelea na zoezi la ununuzi katika vituo vilivyofunguliwa na pia tunaangalia miundombinu mingine ya kuhifadhi mahindi yatakayoendelea kununuliwa,” alisema Kahere.
Alifafanua kuwa ununuzi wa mahindi katika kanda hiyo ulianza Septemba 15, 2026, kwa kufungua vituo vitano vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Ruvuma, kwa kuzingatia upatikanaji wa maghala na urahisi wa kufikika kwa magari yanayosafirisha mazao.
Vituo hivyo ni Lilambwa, kilichopo Manispaa ya Songea; Mkako, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga; Mpandangindo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea; Lituta, katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba; pamoja na Mhangazi.
Kahere alisema idadi ya vituo vilivyofunguliwa msimu huu ni ndogo ikilinganishwa na misimu iliyopita, hatua ambayo imechangiwa na tahadhari ya mvua za El Nino pamoja na umuhimu wa kuhakikisha mahindi yanayonunuliwa yanahifadhiwa katika mazingira salama.
Alisema NFRA imeamua kuelekeza ununuzi katika maeneo yenye maghala na miundombinu inayowezesha mahindi kupelekwa na kuhifadhiwa bila kukabiliwa na hatari ya kuharibika wakati wa usafirishaji au kutokana na changamoto za hali ya hewa.
Kwa mujibu wa Kahere, ghala la Mkako lina uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 za mahindi, huku Lilambwa likiwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 15,000. Maghala ya Mpandangindo, Lituta na Mhangazi yana uwezo wa kuhifadhi tani 1,500 kila moja.
Alisema katika misimu iliyopita, vituo vya ununuzi vilikuwa vikifunguliwa hadi katika baadhi ya vijiji vya ndani ambako mahindi huzalishwa, lakini mfumo huo ulikuwa na changamoto kutokana na ukosefu wa maghala ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi mazao yaliyonunuliwa.
“Tumelazimika kuzingatia maeneo ambayo yanafikika na yenye miundombinu ya kuhifadhi mahindi ili kuhakikisha chakula kinachonunuliwa kinalindwa dhidi ya uharibifu. Hatutaki kununua chakula kingi halafu tukashindwa kukihifadhi vizuri,” alisema.
WITO KWA WAKULIMA KUENDELEA KUIUZIA NFRA MAHINDI
Akizungumzia mwitikio wa wakulima na wafanyabiashara katika vituo vya ununuzi vilivyofunguliwa, Kahere amewahimiza kuendelea kujitokeza kuuza mahindi yao kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), inayotoa fursa ya soko la uhakika kwa bei ya Shilingi 450 kwa kilo.
Alisema NFRA imeweka bei hiyo kwa lengo la kuwapa wakulima na wafanyabiashara fursa nzuri ya kupata kipato kupitia mauzo ya mahindi yao. Bei hiyo ni ya kuvutia ikilinganishwa na bei ya Shilingi 350 hadi 410 kwa kilo inayotolewa na baadhi ya wafanyabiashara wengine.
Kahere alieleza kuwa wakulima na wafanyabiashara wenye akiba ya mahindi wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa kupeleka mazao yao katika vituo vya ununuzi vya NFRA na kupata manufaa ya bei iliyotangazwa.
Aliongeza kuwa kuuza kwa wakati kunawawezesha kupata fedha za kuendeleza shughuli zao za kiuchumi na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kuhifadhi mazao kwa muda mrefu.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa wakulima kuimarisha uwezo wa kuhifadhi mazao yao ili kuongeza fursa za kupata bei nzuri sokoni. Hata hivyo, aliwataka wale ambao tayari wana akiba ya mahindi kujitokeza kwa wingi katika vituo vya NFRA, badala ya kusubiri mabadiliko ya bei ambayo hayana uhakika.
Kahere ametoa wito kwa kuwahimiza wakulima na wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo, akieleza kuwa mauzo kwa NFRA yanachangia kukuza kipato cha wazalishaji, kuimarisha soko la mazao ya kilimo na kuhakikisha upatikanaji wa chakula nchini.
SERIKALI YAWEKA MKAZO KWENYE USALAMA WA CHAKULA
Kahere alisema NFRA inaendelea na juhudi za kuhakikisha inapata kiasi cha mahindi kilichopangwa, huku ikizingatia umuhimu wa kuwa na akiba ya kutosha kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Alisema tahadhari iliyotolewa kuhusu uwezekano wa mvua za El Nino inahitaji maandalizi ya kutosha, hususan katika kuhakikisha chakula kinachopatikana kinahifadhiwa vizuri na kinaweza kutumika pale kinapohitajika.
Aliongeza kuwa bado kuna chakula katika hifadhi za NFRA Kanda ya Songea kinachoweza kusaidia kukidhi mahitaji ya kipindi cha angalau miezi mitatu, ingawa ukubwa wa athari zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa hauwezi kubainishwa kwa uhakika kabla ya kujitokeza.
Kwa mujibu wa Kahere, utaratibu wa hifadhi ya chakula unazingatia umuhimu wa kuwa na akiba inayoweza kusaidia nchi kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa chakula kwa kipindi maalumu, huku ununuzi ukiendelea ili kuongeza kiasi kilichopo.
Alisisitiza kuwa NFRA inaendelea kuchukua hatua za kuongeza ununuzi na kuboresha uwezo wa kuhifadhi mahindi, akieleza kuwa mafanikio ya zoezi hilo yanahitaji ushirikiano wa wakulima, wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta ya kilimo.
Alisema Mkoa wa Ruvuma una nafasi kubwa ya kuchangia kufikiwa kwa lengo la tani 235,000 kutokana na uzalishaji wake wa mahindi, hivyo akatoa wito kwa wenye mazao hayo kutumia fursa ya kuuza kwa NFRA.
Aliongeza kuwa wakala huo utaendelea kufuatilia upatikanaji wa maghala na maeneo mengine yanayoweza kutumika kama vituo vya ununuzi, ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mahindi na kuhakikisha mazao yanayonunuliwa yanahifadhiwa katika mazingira salama.
Kahere alisema lengo kuu ni kuhakikisha nchi ina akiba ya kutosha ya chakula na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zozote zinazoweza kuathiri uzalishaji na upatikanaji wake.
Nao baadhi ya wananchi ambao walikutwa wakiuza mahindi kwenye vituo vya NFRA walieleza kufurahishwa na bei inayotolewa na wakala huyo tofauti na ya walanguzi ambayo ni ndogo.
Mmoja wa wananchi hao, Marianus Mbungu, wa Kijiji cha Litorongi, Kata ya Mkako, Wilaya ya Mbinga alisema wanaendelea kuuza mazao yao kwasababu NFRA inanunua kwa bei ya nzuri ya Sh.450 kwa kilo tofauti na walanguzi ambao wananunua kwa Sh. 350 hadi 400.
Mbungu alisema tofauti na inavyovumishwa na baadhi ya watu, malipo kwa mkulima anapouza mazao yake NFRA yanafanyika ndani ya siku mbili hatua ambayo inamnufaisha mkulima


