Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 KILOMITA 57.1 ZA BARABARA KUPAMBA MJI WA SERIKALI MTUMBA

KILOMITA 57.1 ZA BARABARA KUPAMBA MJI WA SERIKALI MTUMBA


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

MTANDAO  wa barabara za lami wenye urefu wa kilomita 57.1 ni miongoni mwa miundombinu inayobeba sura mpya ya Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, ambao unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Oktoba 30, 2026.

Miundombinu hiyo ni sehemu ya mradi mkubwa unaohusisha majengo ya ofisi za Wizara na taasisi za Serikali, mifumo ya umeme, maji na mawasiliano, kwa lengo la kuimarisha mazingira ya utendaji kazi wa Serikali.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ameeleza hayo jana jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali, akibainisha kuwa uzinduzi huo uliokuwa umeahirishwa kutokana na kifo cha mume wa Rais sasa utafanyika Oktoba 30 mwaka huu.

Mradi huo unahusisha majengo ya ofisi za Wizara 26 na taasisi 11 za Serikali, ambayo yanatarajiwa kutoa mazingira ya kazi kwa watumishi 18,510 katika eneo moja lililopangwa kwa ajili ya shughuli za kiutawala.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 6, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, miundombinu hiyo ni sehemu ya uwekezaji unaolenga kuimarisha huduma na uratibu wa shughuli za Serikali jijini Dodoma.


Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ulianza kwa awamu ya kwanza Novemba 28, 2018, kwa kujenga majengo 23 ya ofisi za muda yaliyokamilika Machi 22, 2019, kabla ya kuanza kwa awamu ya pili Oktoba 2021 iliyolenga kujenga majengo ya kudumu.

Katika awamu hiyo, pamoja na majengo, Serikali imewekeza katika miundombinu wezeshi ikiwemo mfumo wa usambazaji umeme chini ya ardhi wenye urefu wa kilomita 42, unaolenga kuhakikisha majengo yanapata huduma ya nishati.


Huduma za maji safi na uondoshaji wa maji taka pia zimejumuishwa katika mpango wa maendeleo wa eneo hilo ili kukidhi mahitaji ya watumishi na shughuli za kila siku za ofisi za Serikali.


Kwa upande wa mawasiliano, mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) imewekwa ili kurahisisha upashanaji taarifa na mawasiliano kati ya taasisi, huku kamera za CCTV zikilenga kuongeza ulinzi na usalama wa eneo hilo.

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ni miongoni mwa taasisi zinazohusika na ufungaji wa mifumo ya umeme, TEHAMA, viyoyozi, lifti na vifaa vya kielektroniki katika baadhi ya majengo ya Serikali yaliyopo Mtumba.

Mbali na barabara, eneo hilo lina miundombinu mingine ikiwemo Uwanja wa Mashujaa, kituo cha zimamoto na mifumo ya mifereji ya maji inayosaidia kuboresha huduma na kurahisisha shughuli za kila siku.

Mipango ya maendeleo ya mji huo pia imezingatia uhifadhi wa mazingira kupitia upandaji miti, uboreshaji wa mandhari, uvunaji wa maji ya mvua na matumizi ya nishati mbadala, hatua zinazolenga kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali.

Dhana ya mji janja (Smart City) imezingatiwa katika usanifu wa eneo hilo kwa kuunganisha majengo na mifumo ya huduma muhimu kupitia teknolojia za kisasa, ili kuweka mazingira yanayokidhi mahitaji ya utendaji wa Serikali.

Kuwekwa kwa Wizara na taasisi katika eneo moja kunatarajiwa kurahisisha uratibu wa majukumu, kuboresha mawasiliano ya kiutendaji na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika upatikanaji wa huduma baina ya ofisi mbalimbali.

Uzinduzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 30, 2026, utaweka alama nyingine katika maendeleo ya Mji wa Serikali Mtumba, ambao umeandaliwa kuwa eneo muhimu la shughuli za kiutawala na kuongeza mahitaji ya huduma za kiuchumi na kijamii jijini Dodoma.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3