Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 HOMERA ATANGAZA MAPINDUZI YA UMEME VITONGOJINI, AIPONGEZA REA KWA UTEKELEZAJI

HOMERA ATANGAZA MAPINDUZI YA UMEME VITONGOJINI, AIPONGEZA REA KWA UTEKELEZAJI



Na Matukio daima App 

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Homera, amepongeza juhudi za Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy, katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, huku akitangaza kuongezwa kwa kasi ya operesheni ya kuwasha umeme katika kila kitongoji nchini.


Waziri Homera amesema operesheni hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi katika maeneo yote nchini, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hususan katika maeneo ya vijijini.


Akizungumza wakati akiwasha umeme Kitongoji cha Lindi B, Wilaya ya Namtumbo, na Kitongoji cha Nakanyonyo, Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, amesema Wakuu wa Mikoa wataendelea kushiriki katika kuwasha umeme kwenye miradi iliyokamilika ili kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika na huduma hiyo kwa wakati.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza kasi ya matumizi ya miundombinu ya umeme iliyokamilika, huku Serikali ikiendelea kutekeleza miradi mipya katika vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa umeme mkoani Ruvuma, Waziri Homera amesema mkoa huo una jumla ya vitongoji 3,691, ambapo vitongoji 2,235 tayari vimefikiwa na umeme, sawa na takribani asilimia 61 ya vitongoji vyote.

Amesema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 224.7 katika miradi mbalimbali ya umeme inayotekelezwa na REA mkoani humo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua wigo wa upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi.


Kwa mujibu wa Waziri Homera, vitongoji 799 vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya kuviunganishia umeme, huku vitongoji 657 vikiwa bado havijafikiwa na huduma hiyo na havipo katika miradi inayoendelea kutekelezwa.

Amefafanua kuwa kukamilika kwa miradi inayoendelea kutasaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme katika vitongoji vya Mkoa wa Ruvuma kutoka asilimia 61 ya sasa hadi takribani asilimia 82.

Amesema ongezeko hilo linatarajiwa kufungua fursa zaidi za shughuli za kiuchumi, ikiwemo biashara, uzalishaji mali na utoaji wa huduma za kijamii, hivyo kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo ya vijijini.

Aidha, Waziri Homera amewataka wananchi kuendelea kuiombea Wizara ya Nishati ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha azma ya kufikisha umeme kila kitongoji inafikiwa.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini imeendelea kuongezeka na kwamba Wakala  hautarudi nyuma katika kutimiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma ya umeme.

Mhandisi Saidy amesisitiza kuwa Wakala utaendelea kuongeza juhudi za kusogeza huduma ya umeme katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa, sambamba na kufungua fursa mpya za kiuchumi, kuongeza uzalishaji na kuboresha ustawi wa wananchi wa vijijini.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3