Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 HESLB YATENGA SH1.06 TRILIONI KWA MIKOPO YA ELIMU YA JUU

HESLB YATENGA SH1.06 TRILIONI KWA MIKOPO YA ELIMU YA JUU

Na Matukio DaimaMedia 

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetenga kiasi cha TSh1.06 trilioni kwa ajili ya mikopo na ufadhili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2026/2027 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.6 ikilinganishwa na Sh916.7 bilioni zilizotengwa mwaka uliopita.

Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salam na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill M. Kiwia,wakati wa mkutano na wahariri na Waandishi wa vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa masomo 2022/2023 hadi 2026/2027.

Amesema kuwa, bajeti hiyo inatarajiwa kunufaisha wanafunzi wasiopungua 300,000, ikilinganishwa na wanafunzi 289,932 walionufaika mwaka 2025/2026.

Aidha, katika awamu hiyo, wanafunzi 165,775 wamepangiwa mikopo na ruzuku zenye thamani ya Sh 535.7 bilioni, ambapo kati yao, wanafunzi 74,769 wa shahada ya kwanza wamepangiwa mikopo ya Sh246.88 bilioni, huku wanafunzi 8,538 wa stashahada wakipangiwa Sh22.9 bilioni.

Aidha, wanafunzi 873 wa Samia Scholarship wamepangiwa ruzuku ya Sh4.5 bilioni. Kwa ujumla, wanafunzi 2,738, wakiwemo wanafunzi wapya 1,000, wanatarajiwa kunufaika na ufadhili huo katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).

Ameongeza kuwa, katika ngazi ya stashahada, jumla ya wanafunzi 24,978 watagharimiwa masomo yao, wakiwemo wanafunzi 14,000 wa mwaka wa kwanza. HESLB pia imeongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza kutoka Sh8,500 hadi Sh10,000 kwa siku.

Kwa upande wa urejeshaji wa mikopo, HESLB imekusanya Sh1.91 trilioni kati ya Sh2.77 trilioni zilizostahili kukusanywa kuanzia mwaka 2005/2006 hadi Juni 2026, sawa na asilimia 69 ya fedha zilizotarajiwa kurejeshwa.

"Makusanyo yameendelea kuongezeka katika miaka ya karibuni, kutoka Sh177 bilioni mwaka 2023/2024 hadi Sh194 bilioni mwaka 2024/2025. Mwaka 2025/2026, bodi ilikusanya Sh235.5 bilioni, sawa na asilimia 107 ya lengo la Sh220 bilioni"amesema Dkt Kiwia.


Ameongeza kuwa, katika kuhakikisha bodi hiyo inaendelea mbele Kwa mwaka wa masomo 2026/2027, HESLB inalenga kukusanya tena Sh220 bilioni kupitia kampeni ya #Kiduchu Fresh Tunasonga, iliyoanzishwa Aprili 2026.

Katika kuimarisha utoaji wa huduma, bodi imezindua Mpango Mkakati wa Sita wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031 baada ya kutekeleza Mpango Mkakati wa Tano kwa ufanisi wa asilimia 82. Hatua hiyo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuhakikisha angalau asilimia 25 ya Watanzania wanapata elimu ya juu na mafunzo ifikapo mwaka 2050.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3