Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TANZANIA YAPIGA HATUA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO, KUWANIA KITI BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA (UN), YASUKUMA MBELE AJENDA YA AFRIKA

TANZANIA YAPIGA HATUA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO, KUWANIA KITI BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA (UN), YASUKUMA MBELE AJENDA YA AFRIKA

 
Tanzania imetangaza azma yake ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030, huku ikiahidi kupeleka katika chombo hicho sauti imara ya Afrika na kusukuma mbele diplomasia ya kuzuia migogoro, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani na mageuzi ya operesheni za kulinda amani.
 
Msimamo huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mjadala wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, unaofanyika jijini New York, Marekani.
 
Mhe. Ndejembi amesema Tanzania ikichaguliwa itatoa kipaumbele kwa diplomasia ya kuzuia migogoro kabla haijawa vita, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani, kuimarisha nafasi ya wanawake katika ulinzi na ujenzi wa amani, kuongeza ushiriki wa vijana katika ajenda za amani na usalama, pamoja na kusukuma mbele mageuzi ya operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani.
 
Tanzania imesema dhamira hiyo imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika (AU), huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika Juni 2028.
 
Katika hotuba ya Makamu wa Rais, Tanzania imeweka wazi msimamo kwamba Umoja wa Mataifa unapaswa kuendelea kufanyiwa mageuzi ili kuimarisha misingi ya haki, usawa na uwakilishi wenye uwiano, badala ya mfumo wa kimataifa kuendelea kuakisi zaidi nguvu na ushawishi wa mataifa machache.
 
Tanzania imesisitiza kuwa mageuzi hayo ni muhimu katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na migogoro na vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa, kasi ya maendeleo ya Akili Mnemba (AI), pamoja na changamoto za usalama wa nishati.
 
 
Makamu wa Rais amesema, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuongeza kiwango cha uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022. Amesema uzoefu katika hilo unaonyesha kuwa uwekezaji katika miradi inayotekelezeka na kuweka ustawi wa watu mbele, maendeleo yanaweza kuhama kutoka hatua ya ahadi hadi matokeo yanayoonekana na kupimika.
 
Amesema ni kwa msingi huo ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alikubali jukumu la kuwa kinara wa masuala ya Afya ya Mama na Mtoto kwa niaba ya Umoja wa Afrika. Chini ya uongozi wake, Tanzania imefanikiwa  kupunguza vifo vya akina mama kwa asilimia 80 ndani ya kipindi cha miaka saba pekee. Tanzania inalenga kufikia malengo ya "Sifuri Tatu" (Three Zeros), ambayo ni: Kutokuwepo kwa vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kuzuilika;

 kutokuwepo kwa uzazi unaofanyika majumbani; na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo. Amesema uzoefu unaonyesha kuwa hilo ni lengo ambalo Afrika inaweza kulifikia kwa mafanikio, lakini litahitaji uongozi thabiti wa kisiasa, rasilimali fedha za kutosha, na ushirikiano imara zaidi. Hivyo, amehimiza Jumuiya ya Kimataifa kuungana nasi katika kulisukuma mbele ajenda hiyo.
 
Tanzania pia imesisitiza umuhimu wa nchi zinazoendelea kupewa sauti kubwa zaidi katika taasisi na mifumo ya kimataifa inayofanya maamuzi ya kifedha yanayoathiri uchumi wake wa muda mrefu wa maendeleo, Tanzania imewasilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kama msingi wa kujenga uchumi jumuishi, shindani na wenye uwezo wa kustahimili misukosuko, kupitia uwekezaji katika watu, miundombinu yenye tija, teknolojia, ubunifu, wanawake na vijana.
 
Makamu wa Rais amesema ni muhimu kufanyika kwa mageuzi kwenye mfumo wa fedha wa kimataifa ili nchi zinazoendelea ziweze kupata rasilimali zinazohitajika kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Amesema Tanzania inasisitiza kuongezeka kwa mikopo yenye masharti nafuu,

 kuhamasishwa kwa uwekezaji wa sekta binafsi, kurahisishwa kwa upatikanaji wa fedha za maendeleo na tabianchi na nchi zinazoendelea kupewa sauti kubwa katika maamuzi ya kifedha duniani.
 
Katika ajenda ya mabadiliko ya tabianchi, Tanzania imeeleza wasiwasi kuhusu pengo kati ya kiwango cha uzalishaji wa gesi chafuzi duniani na fedha zinazotolewa kusaidia nchi zinazoathirika kukabiliana na madhara yake.
 
Tanzania imesisitiza kuwa nchi zinazochangia kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa gesi chafuzi zinapaswa kubeba wajibu mkubwa zaidi katika kugharamia hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
 
 
Katika kueleza mkakati wake wa mpito kuelekea nishati safi, Tanzania imetaja Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, miradi ya nishati ya jua na upepo yenye jumla ya megawati 650, pamoja na mipango ya kuzalisha megawati 130 za nishati ya jotoardhi.
 
Pia imetaja uwekezaji katika reli ya umeme na lengo la kufikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika asilimia 80 ya kaya ifikapo mwaka 2034.
Katika eneo la diplomasia ya kimataifa, Makamu wa Rais amesema Tanzania inapinga matumizi ya vikwazo vya upande mmoja vinavyowekwa na baadhi ya mataifa dhidi ya mengine, ikisema hatua hizo zinaweza kudhoofisha mamlaka ya nchi, kuathiri maendeleo na kupunguza uwezo wa wananchi kunufaika kikamilifu na haki zao.
 
Tanzania imeeleza mshikamano wake na Cuba, Zimbabwe na mataifa mengine yanayokabiliwa na vikwazo hivyo, huku ikitoa wito wa kuchukuliwa hatua za makusudi kuelekea kuondolewa kwa vikwazo bila masharti.
 
Kuhusu hali ya Gaza na Mashariki ya Kati, Tanzania inasisitiza umuhimu wa kuwalinda raia, kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wanaohitaji bila vikwazo na kurejesha diplomasia kuwa njia kuu ya kutafuta amani ya kudumu.
 
Kwa ujumla, ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeunganisha ajenda ya kitaifa ya maendeleo na hoja pana kuhusu nafasi ya Afrika katika mfumo wa kimataifa.
 
Tanzania imesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa haupaswi kuwa jukwaa linaloakisi pekee uwiano wa nguvu duniani, bali taasisi inayosimamia haki, mshikamano, usawa na maendeleo kwa mataifa yote.
 
Ni msimamo unaoweka bayana ajenda ambayo Tanzania inakusudia kuibeba katika safari yake ya kuwania nafasi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030: kuimarisha sauti ya Afrika, kuzuia migogoro, kutetea suluhu za amani na kusukuma mageuzi ya mfumo wa kimataifa ili uwe na uwakilishi wenye uwiano zaidi.
 
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
New York – Marekani
23 Septemba 2026.




 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3