DKT. MWIGULU AHIMIZA USHIRIKIANO WA KIKANDA KUDHIBITI MAGONJWA YA MIFUGO
Sep 23, 2026
*_▪︎ EU kuwekeza Euro milioni 50 kusaidia kutokomeza sotoka barani Afrika_*
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na FAO, Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH), Umoja wa Afrika, jumuiya za kikanda, na wadu wengine katika kuimarisha uwekezaji na mifumo ya kudhibiti magonjwa ya mifugo kwa lengo la kuchangia kutokomeza Sotoka ifikapo mwaka 2040.
“Tunataka kuona uwekezaji wenye nguvu zaidi, unaotabirika na endelevu. Umiliki wa kitaifa na ufadhili wa ndani lazima viwe msingi, vikisaidiwa na FAO, WOAH, Umoja wa Afrika, jumuiya za kikanda, taasisi za fedha za kimataifa, washirika wa maendeleo na sekta binafsi.”
“Tunapaswa kuondoka katika hatua zilizotawanyika na kuelekea kwenye mifumo ya kudumu; kutoka mipango ya kitaifa pekee kwenda ushirikiano wa kikanda; na kutoka ahadi kwenda kwenye matokeo yanayoweza kupimika,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Alisema hayo jana, (Jumanne, Septemba 22, 2026) jijini Roma, Italia, wakati akishiriki mjadala wa ngazi ya juu kuhusu uwekezaji katika kutokomeza Sotoka na kudhibiti Ugonjwa wa Miguu na Midomo kwenye Mkutano wa Kimataifa ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kuhusu utekelezaji wa Afya Moja katika mifumo ya chakula na kilimo.
Alisema chanjo pekee haitoshi, bali Tanzania inahitaji maabara zinazofanya kazi, mifumo madhubuti ya ufuatiliaji, usambazaji wa chanjo wa uhakika, utambuzi wa mifugo, wataalamu wenye ujuzi na ushirikiano baina ya nchi na nchi hasa kwenye maeneo ya mipakani.
Akizungumzia umuhimu wa ushirikiano wa kikanda, Dkt. Mwigulu alisema magonjwa ya mifugo hayaheshimu mipaka ya nchi, na kubainisha kuwa wakati nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zikijadili hatua za kuelekea shirikisho, wanyama tayari wameungana kwa kasi zaidi.
“Wakati nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiendelea kujadili namba ya kuingia katika mfumo wa shirikisho, wanyama tayari wameungana haraka kuliko sisi,” alisema.
Akifungua mlango wa kuchangia mada kwenye mjadala huo, Balozi wa Umoja wa Ulaya jijini Roma na Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja huo katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya Roma, Dkt. Martin Selmayr, alisema Umoja wa Ulaya unaandaa uwekezaji mpya wa Euro milioni 50 kwa ajili ya awamu ya pili ya mpango wa kutokomeza Sotoka barani Afrika.
Balozi Selmayr alisema uwekezaji huo unalenga kuongeza nguvu katika juhudi za kutokomeza ugonjwa huo na kuwa kichocheo kwa nchi husika, taasisi za fedha za maendeleo, sekta binafsi na washirika wengine kuongeza uwekezaji katika programu za kitaifa za kutokomeza sotoka.
“Umoja wa Ulaya unaamini kuwa uwekezaji huo haupaswi kuishia katika kampeni nyingine ya chanjo pekee, bali unapaswa kusaidia pia kuimarisha huduma za mifugo, uzalishaji na ubora wa chanjo, ushirikiano wa sekta binafsi pamoja na hatua za pamoja za kukabiliana na magonjwa yanayovuka mipaka,” alisisitiza.
Naye, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Godfrey Magwenzi, alisema afya ya wanyama ni uwekezaji wa kimkakati katika usalama wa chakula, maendeleo ya uchumi na ustahimilivu, akisisitiza umuhimu wa uwekezaji wa muda mrefu katika kutokomeza sotoka.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uzalishaji wa Wanyama wa Chad, Prof. Abderrahim Awat Atteib, alisema juhudi za kutokomeza ugonjwa huo zinahitaji ufadhili endelevu na unaotabirika ili kuzuia ugonjwa huo kurejea katika maeneo ambayo tayari yamedhibitiwa.
Naye, Dkt. Samuel Thevasagayam, Mkurugenzi wa Timu ya Mifugo wa Taasisi ya The Gates Foundation, alisema mafanikio ya kutokomeza sotoka yanahitaji umiliki wa Serikali, ushiriki wa wafugaji na sekta binafsi, pamoja na matumizi ya sayansi na ushahidi katika kupanga na kutekeleza hatua za kudhibiti ugonjwa huo.




