RC HAMDUN AWATAKA WATUMISHI KUFATA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU
.
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamdun, amewataka watumishi wa umma katika Wilaya ya Kwimba kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa hatakuwa na utani kwa watumishi watakaoshindwa kutekeleza maagizo na maelekezo ya Serikali.
CP Hamdun ametoa kauli hiyo kufatia hatua ya mkuu wa Wilaya ya Kwimba Ng'wilabuzu Ludigija kumwamuru Mkurugenzi wa halmashauri hiyo pamoja na wakuu idara wote kuripoti kwa mkuu wa polisi wa Wilaya (OCD) kufatia hatua yao ya kukaidi mara kadhaa agizo la kushiriki zoezi la usafi wa mazingira.
Maagizo hayo ameyatoa leo septemba 28, 2026 wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Wilaya ya Kwimba, ambapo amesisitiza umuhimu wa watumishi kutekeleza kikamilifu maelekezo yanayotolewa na viongozi katika ngazi mbalimbali kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Amesema watumishi wa umma, viongozi na watendaji katika kila ngazi wanapaswa kuhakikisha wanafata maagizo na maelekezo yanayotolewa na Serikali nakutekelezwa kwa wakati na kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Akitolea mfano wa zoezi la usafi wa mazingira, CP Hamdun amesema agizo la kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi linatoka Serikalini na limekuwa likishushwa kutoka ngazi ya Taifa hadi mkoa na wilaya, hivyo hakuna sababu kwa watumishi kushindwa kulitekeleza.
Aidha amefafanua kuwa kutokuwepo kwa baadhi ya watumishi katika utekelezaji wa majukumu yaliyokubaliwa kunatoa taswira ya kutokuwepo kwa ushirikiano na uwajibikaji miongoni mwa watendaji wa Serikali.
“Hawezekani Mkuu wa Wilaya kufika kwenye zoezi ambalo tulikubaliana, halafu akitazama kulia na kushoto anajikuta yuko peke yake niwaombe watumishi wa umma na Mkurugenzi Mtendaji ambaye ni mamlaka ya nidhamu, pamoja na Baraza la Madiwani, kusimamia nidhamu ya watendaji wa halmashauri,” amesema CP Hamdun.
Amesema ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kutenda kwa mujibu wa taratibu, akizingatia sheria za utumishi wa umma, maelekezo na miongozo ya Serikali pamoja na maadili ya viongozi na watendaji.
CP Hamdun amemtaka Katibu Tawala wa Wilaya kuhakikisha watumishi walio chini ya mamlaka yake wanafuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, huku akisisitiza kuwa suala hilo halipaswi kufanyiwa mzaha.
“Sitakakuwa na utani na mtu yeyote yule. Katibu Tawala Mkoa, hakikisha jambo hili unalisimamia. Kama unaona huwezi kufanya kazi, una shughuli zako nyingine, andika notisi ya saa 24 kuacha kazi, maana tunao Watanzania vijana wengi wenye sifa na uwezo wa kuajiriwa,” amesema.
Aidha, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, ambaye ni mamlaka ya nidhamu kwa watumishi, pamoja na Baraza la Madiwani kupitia uongozi wake, kuhakikisha nidhamu ya watendaji inasimamiwa na watumishi wanawajibika katika maeneo yao ya kazi
Hata hivyo ameeleza kuwa utekelezaji wa maagizo ya Serikali unapaswa kuwa sehemu ya majukumu ya kila siku ya mtumishi wa umma, huku kila mmoja akitakiwa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria na taratibu bila kusubiri kusukumwa na viongozi.
Amesema usafi wa mazingira nao unapaswa kuwa sehemu ya utamaduni wa wananchi wa Wilaya ya Kwimba, ambapo pamoja na kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, zoezi hilo linapaswa kwenda sambamba na upandaji miti na uanzishaji wa bustani za kupumzikia ili kuboresha mazingira ya miji na maeneo ya makazi.



