RAIS DKT. MWINYI AFUNGUA IJITIMAI BUNGI, ATOA WITO WA AMANI NA MALEZI BORA
Sep 18, 2026
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza viongozi wa dini ya Kiislamu kuendelea kusisitiza umuhimu wa amani, upendo, umoja na mshikamano, pamoja na kuimarisha malezi ya watoto na vijana katika misingi ya maadili mema.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 18 Septemba 2026, baada ya Sala ya Ijumaa, alipofungua rasmi Ijitimai ya Jumuiya ya Tabligh Markaz Zanzibar katika eneo la Bungi, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kuwakumbusha waumini mambo ya kheri, kuimarisha maadili na kujenga familia na jamii zinazozingatia mafundisho ya dini.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto na vijana, hususan katika matumizi ya mitandao ya kijamii, ili kuhakikisha wanapata maudhui yenye manufaa na kujengeka katika maadili mema.
Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza wananchi kuchukua tahadhari kufuatia taarifa za mamlaka kuhusu mvua kubwa zinazotarajiwa, huku akiwataka viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari na kumuomba Mwenyezi Mungu kuliepusha Taifa na majanga.
Akizungumzia amani na utulivu, Rais Dkt. Mwinyi amesema mazingira hayo yanaendelea kutoa fursa kwa shughuli za kidini, kijamii na kiuchumi, na amesisitiza umuhimu wa wananchi na viongozi wa dini kushirikiana katika kuimarisha mshikamano wa jamii.
Ijitimai hiyo imewakutanisha waumini kutoka mataifa mbalimbali duniani na itafanyika kwa muda wa siku tatu, ikiwa na shughuli za mafundisho ya dini, dua na kuimarisha umoja, mshikamano na maadili mema katika jamii.



