MIL.71 KUONDOA MSONGAMANO KITUO CHA AFYA NGURUKA
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Halmashauri ya wilaya uvinza mkoani Kigoma imetumia kiasi cha shilingi milioni 71.6 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba sita vya kujifungua wajawazito na wodi yenye vitanda 15 kwenye kituo cha afya Nguruka ili kukabiliana na wimbi kubwa la mama wajawazito wanaojifungulia kwenye kituo hicho.
Sambamba na ujenzi wa wodi hizo pia halmashauri imekarabati jengo lililokuwa likitumika awali katika kituo hicho kilichoanza kutumika mwaka 1976 na kwamba mradi huo unatokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya mama wajawazito wanaojifungulia kwenye kituo hicho cha afya.
Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Nguruka, Joseph George akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru, Wazo Mwang’onda alisema kuwa WATOTO 400 wanazaliwa kila mwezi kwenye kituo hicho kikiwa ni moja ya vituo vinavyokabiliwa na idadi kubwa ya mama wajawazito wanaofika kituo hapo kujifungua.
George alisema kuwa hali hiyo ilikifanya kituo hicho kuzidiwa na idadi kubwa ya watu ambayo ilikuwa haiendani na hali halisi ya utoaji huduma hasa majengo na ndipo halmashauri iliamua kutumia mapato ya ndani kujenga wodi ya kujifunguliwa wajawazito na kulaza wagonjwa.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa wilaya Uvinza, Dinna Mathamani alisema kuwa idadi kubwa ya watu katika eneo hilo linachangia pia idadi kubwaya watu wanaojifungua lwenye kituo hicho ambapo hata maboresho yamekuwa yakifanyika kila wakati hali ya majengo,idadi ya watu viwe na uwiano katika utoaji huduma.
Akizindua kituo hicho kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru, Wazo Mwang'onda alisema kuwa serikali imedhamiria kuboresha utoaji huduma za afya ikiwemo ya Mama mjamzito na watoto ili kupata mtoto isiwe adhabu kwa Mtanzania.


