MADEBE NA MAKOP0 SIYO VIPIMO, WMA YATOA ONYO KWA WAFANYABIASHARA
Sep 18, 2026
Dodoma
Wakala wa Vipimo (WMA) umewataka wafanyabiashara na wananchi kuacha kutumia madebe, makopo na vyombo vingine visivyo na viwango kama vipimo vya kupimia bidhaa, ukisisitiza kuwa matumizi ya vifaa hivyo ni kinyume cha sheria.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Mark Kihula, amesema hayo leo, Septemba 18, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO kuhusu utekelezaji wa shughuli za Wakala katika mwaka wa fedha 2025/2026 na mwelekeo wa mwaka 2026/2027.
Kihula amesema madebe na makopo hayawezi kutumika kama vipimo kwa kuwa havihakikishi usawa wa kiasi cha bidhaa kinachouzwa na kinacholipiwa na mlaji.
“Madebe, makopo na vyombo vingine siyo vipimo. Sheria inakataza matumizi yake kama vipimo. Tunatoa elimu na pia tunachukua hatua kwa wanaojihusisha na upimaji wa namna hii,” amesema.
Amesema WMA itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia mizani yenye usahihi, huku akiwahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kununua bidhaa zinazopimwa kwa mizani ili kuhakikisha wanapata kiasi kinacholingana na fedha wanazolipa.
“Jukumu letu kama Wakala wa Vipimo ni kuhakikisha kuna usawa,” amesema Kihula.
Kwa mujibu wa Kihula, katika kuhakikisha huduma bora za vipimo zinawafikia wananchi, WMA ina ofisi katika mikoa yote ya Serikali Tanzania Bara zinazotoa huduma za uhakiki, ukaguzi na usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo kwa wafanyabiashara na wananchi.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026, WMA ilifanya uhakiki wa jumla ya vipimo 1,166,995, sawa na asilimia 92ya lengo la kuhakiki vipimo 1,269,957.
Katika kuhakikisha wakulima wanapata kipato kinachoendana na mazao wanayouza, Kihula amesema WMA imeendelea kukagua mizani inayotumika kupimia mazao ya kimkakati, ikiwemo korosho, pamba, kahawa na ufuta katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi, Kigoma, Katavi na Kanda ya Ziwa.
Amesema katika msimu wa mwaka 2025/2026, WMA imewezesha kuanza kutumika kwa mizani janja (anti-tampering scales) inayomsaidia mkulima kufahamu kiasi cha mazao aliyouza mara baada ya kupima, pamoja na kuiwezesha Wakala kupata taarifa endapo mzani utachezewa kinyume na taratibu.
Katika upande wa ukaguzi wa maeneo ya biashara, Kihula amesema WMA ilipanga kufanya kaguzi 4,000 za kawaida na za kushtukiza katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 30, 2026.
Hata hivyo, Wakala ilifanya jumla ya kaguzi 5,015, sawa na asilimia 125 ya lengo, huku vipimo vilivyokaguliwa kwa wingi vikiwa ni pampu za mafuta na mizani inayotumika katika biashara za rejareja.
Aidha, amesema WMA imeendelea kukagua bidhaa zilizofungashwa zinazozalishwa nchini pamoja na zinazoingia kutoka nje, ikiwemo vifaa vya ujenzi kama tiles, saruji, nondo na mabati, pamoja na vinywaji na vyakula.
Katika kipindi hicho, jumla ya bidhaa 21,262 zilizozalishwa nchini na shehena 17,774 za bidhaa zilizoingia kutoka nje zilikaguliwa, kwa lengo la kuhakikisha walaji wanapata bidhaa zenye kiasi kilichoainishwa na mzalishaji.
Kuhusu mafuta yanayoingia nchini, Kihula amesema WMA imeendelea kuhakiki kiasi cha petroli, dizeli, mafuta ya ndege na mafuta ya kula yanayoingia kupitia Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
Amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 30, 2026, Wakala ilihakiki jumla ya lita 11,995,743,266 za mafuta zilizowasili kwa meli 183.
Kati ya kiasi hicho, lita 3,702,807,940.56 zilikuwa petroli, lita 7,382,184,171.85 dizeli, lita 500,249,473.78 mafuta ya ndege na lita 410,501,680 mafuta ya kula.
Kihula amesema WMA itaendelea kuhakikisha usahihi wa mizani za aina mbalimbali, pampu za kuuzia mafuta, matenki ya kuhifadhia mafuta na mita nyingine, pamoja na kuimarisha ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa na usimamizi wa kiasi cha mafuta yanayoingia nchini.
Aidha, amesema Wakala itaendelea kuboresha na kupanua matumizi ya mfumo wa WMA-MIS na huduma nyingine za kidijitali ili kuwawezesha wananchi na wafanyabiashara kupata huduma za uhakiki na ukaguzi kwa urahisi bila kulazimika kufika ofisini.

