HARVEST MISSION INTERNATIONAL UNIVERSITY CHAWAKARIBISHA WANAFUNZI WA TANZANIA KUJIUNGA KUPATA ELIMU
Mkurugenzi wa Harvest Mission International University Texas, Marekani Nchini Tanzania Prof. Issack Yona Mpema (kulia) akimpongeza mkurugenzi wa Matukio Daima Media Francis Godwin jana baada ya kutembelea ofisi za Matukio Daima Media mjini Iringa leo
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
MKURUGENZI wa Harvest Mission International University Texas, Marekani Nchini Tanzania Prof. Issack Yona Mpema, amewakaribisha wanafunzi wanaotarajia kujiunga na chuo hicho kuchukua kozi mbalimbali za dini na zisizo za dini zinazotolewa kwa njia ya mtandao.
Prof. Mpema ametoa mwaliko huo leo asubuhi wakati akizungumza katika kipindi cha Press kupitia Matukio Daima Media, alisema chuo hicho kimejizatiti zaidi katika kutoa elimu ya dini, huku pia kikitoa fursa ya kusoma kozi nyingine kwa njia ya mtandao.
“Ni chuo cha dini, lakini kina mamlaka ya kutoa kozi za secular kwa njia ya kimtandao duniani kote. Makao makuu yetu yapo Texas ambako tuna majengo kabisa, hivyo ni chuo,” amesema Prof. Mpema.
Alisema Harvest Mission International University ni chuo cha kimataifa kinachotoa elimu ya ngazi za juu, ikiwemo Shahada za Uzamili (Master’s) na Uzamivu (PhD), kwa lengo la kuongeza fursa za elimu na kukuza taaluma kwa wanafunzi na wataalamu.
Kwa mujibu wa Prof. Mpema, chuo hicho hakipo kwa lengo la kushindana au kupambana na vyuo vya ndani ya Tanzania, bali kuchangia juhudi za kuongeza idadi ya wataalamu wenye elimu ya juu nchini.
Alisema anaamini kuwepo kwa taasisi nyingi zinazotoa fursa za elimu kunaweza kusaidia Tanzania kuzalisha wataalamu wengi zaidi katika maeneo mbalimbali na kuchangia maendeleo ya taifa.
Aidha, Prof. Mpema amesema yeye pia ni mwakilishi katika masuala ya amani kimataifa, nafasi ambayo amesema anaitumia kuendelea kuhimiza umuhimu wa amani na utulivu nchini Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla.
“Ninatamani sana nchi yetu tuishi kwa amani.
Tanzania iwe mahali pa kuishi, Afrika iwe mahali pa kuishi na dunia kwa ujumla iwe mahali salama pa kuishi. Kote tuishi kwa amani na utulivu,” amesisitiza Prof. Mpema.
Katika hatua nyingine, aliwakaribisha watu wanaotaka kujiunga na chuo hicho kufanya udahili na usajili kwa njia ya mtandao, huku akieleza kuwa wanaohitaji maelezo zaidi wanaweza kufika katika ofisi zake zilizopo maeneo ya Songas, jijini Dar es Salaam.
Alisema milango iko wazi kwa wanaotaka kusoma elimu ya dini pamoja na kozi nyingine zinazotolewa na chuo hicho kwa mfumo wa mtandao.

