FAHAMU LISHE BORA NA MAKUNDI SITA YA VYAKULA
Na Bibi Maendeleo, Irene Samora
Lishe bora ni ulaji wa mlo kamili unaotokana na makundi yote sita ya vyakula. Mlo kamili huupatia mwili virutubisho vinavyohitajika kwa ajili ya kutoa nguvu, kujenga mwili, kuimarisha kinga na kuuwezesha kufanya kazi zake vizuri.
Makundi sita ya vyakula ni haya yafuatayo:
1. Vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi
Vyakula hivi ni chanzo kikubwa cha wanga, ambao huupa mwili nguvu na nishati. Mifano yake ni mahindi, ndizi mbichi na za kupikwa, mihogo, ngano, mchele na viazi.
Ili mwili uweze kufanya shughuli mbalimbali za kila siku, unahitaji kupata vyakula vya kundi hili kwa kiwango kinachofaa.
2. Vyakula vya asili ya wanyama
Vyakula hivi ni chanzo muhimu cha protini, ambayo husaidia kujenga mwili, kutengeneza seli mpya na kukarabati tishu zilizoharibika.
Mifano ya vyakula vya kundi hili ni nyama ya ng’ombe, kuku, samaki, mayai, senene, kumbikumbi na maziwa.
3. Vyakula vya jamii ya mikunde na mbegu
Kundi hili linajumuisha maharage, kunde, mbaazi, choroko, dengu na njegere. Vyakula hivi vina protini pamoja na madini mbalimbali yanayohitajika katika mwili.
Virutubisho vinavyopatikana katika vyakula hivi husaidia kujenga mwili, kutengeneza seli na kuimarisha afya kwa ujumla.
4. Mboga
Mboga ni chanzo muhimu cha vitamini na madini ambayo husaidia kuulinda mwili dhidi ya magonjwa.
Mifano yake ni tembele, mchicha, spinachi, mlenda, majani ya maboga, kisamvu, kabichi, majani ya kunde, bamia, nyanya chungu, mashona-nguo, karoti, hoho na bilinganya.
Mboga zinapaswa kuandaliwa kwa usafi na zisipikwe kwa muda mrefu sana, kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kupunguza baadhi ya virutubisho vyake.
5. Matunda
Matunda ni chanzo cha vitamini na madini ambayo husaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuukinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Mifano ya matunda ni tikitimaji, maembe, zabibu, nanasi, parachichi, mapera, ndizi mbivu na papai. Pia yapo matunda ya porini, kama vile furu, ukwaju, ubuyu na embe ng’ongo.
Ni muhimu kula matunda mbalimbali mara kwa mara ili kuupatia mwili virutubisho vinavyohitajika.
6. Mafuta
Mafuta yanayotokana na mimea, kama vile ufuta na alizeti, ni muhimu kwa kuupa mwili nguvu na nishati. Mafuta pia husaidia mwili kufyonza baadhi ya vitamini, ikiwemo vitamini A, D, E na K.
Hata hivyo, licha ya umuhimu wake, mafuta yanapaswa kutumiwa kwa kiasi kidogo. Matumizi ya mafuta mengi yanaweza kuchangia kuongezeka kwa uzito wa mwili na hatari ya kupata shinikizo la damu pamoja na magonjwa mengine.
Faida za lishe bora
Lishe bora ina faida nyingi kwa afya ya binadamu. Baadhi ya faida hizo ni:
1:Hutengeneza seli mpya za mwili.
2:Hukarabati tishu zilizoharibika.
3:Husaidia kutengeneza vichocheo vya mwili.
4:Huchangia ukuaji mzuri wa akili na mwili.
5:Huupa mwili nguvu na joto.
6:Husaidia kuzuia baadhi ya magonjwa, ikiwemo saratani.
7:Husaidia umeng’enyaji wa chakula na kudhibiti kiwango cha sukari mwilini.
8:Husaidia mwili kupata nguvu za kufanya shughuli mbalimbali.
9:kutengeneza baadhi ya vichocheo muhimu mwilini.
10:Husaidia ufyonzwaji wa vitamini A, D, E na K.
11:Hulinda mwili dhidi ya magonjwa.
12:Husaidia kuimarisha mifupa na meno.
13:Husaidia kupambana na upungufu wa damu kupitia madini ya chuma.
14:Huimarisha kinga na afya ya mwili kwa ujumla.
Madhara ya kukosa lishe bora
Mtu asipopata lishe bora anaweza kukabiliwa na madhara mbalimbali ya kiafya, yakiwemo:
1:Mwili kudhoofika.
2:Kupoteza nguvu mwilini.
3:Kuongezeka kwa hatari ya kupata magonjwa sugu na maambukizi.
4:Udhaifu na uchovu wa mara kwa mara.
5:Kudhoofika kwa kinga ya mwili.
6:Kudumaa kwa watoto kimwili na kiakili.
7:Magonjwa ya mifupa na misuli.
8:Matatizo ya afya ya akili.
Lishe bora na afya njema
Lishe bora ni moja ya nguzo muhimu za afya njema. Mbali na kula chakula bora, mtu anatakiwa kufanya mazoezi ya viungo, kunywa maji safi na salama, kupata mwanga wa jua, kuvuta hewa safi na kupata muda wa kutosha wa kupumzika.
Binadamu anahitaji chakula ili aweze kuishi, kukua na kufanya shughuli zake za kila siku. Hata hivyo, chakula kinapaswa kuchaguliwa, kuandaliwa na kuhifadhiwa kwa usafi na umakini mkubwa.
Kwa hiyo, chakula kiwe dawa kwa mwili. Kisipochaguliwa na kuandaliwa vizuri kinaweza kuwa chanzo cha matatizo ya kiafya. Tafiti zinaonyesha kuwa takribani asilimia 35 ya visa vya saratani vinaweza kuhusishwa na ulaji usiofaa.
Kila mtu anapaswa kuhakikisha anakula mlo kamili wenye vyakula kutoka katika makundi yote sita kwa kiasi kinachofaa. Lishe bora ni msingi wa ukuaji mzuri, nguvu, kinga imara na maisha yenye afya.
Fuatilia kipindi cha bibi Maendeleo kila siku kupitia matukio Daima Tv kwa mawasiliao piga 0656285926/0754026299 ⬇️⬇️⬇️
