WATU WANNE WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA WIZI WA MBUZI MVOMERO
Aug 1, 2026
Na Matukio Daima Media, Morogoro
WATU wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa mbuzi 53, ambapo 32 kati yao wamepatikana wakiwa mikononi mwa watuhumiwa hao wilayani Mvomero.
Watuhumiwa hao wamekamatwa Julai 31, 2026, majira ya saa 2 usiku katika eneo la Majichumvi, Kitongoji cha Sokoine Vijana, Kijiji cha Wami Luhindo, Kata ya Dakawa, Wilaya ya Mvomero.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, mbuzi hao wanadaiwa kuibwa Julai 24, 2026 katika Kijiji cha Kimambila, Kata ya Lubungo, Tarafa ya Mlali wilayani Mvomero, katika zizi la Majaliwa John Gombo (48), mfugaji na mkazi wa Dar es Salaam.
Polisi imesema kuwa watuhumiwa hao wamekiri kuhusika na tukio hilo wakati wa mahojiano ya awali, huku uchunguzi zaidi ukiendelea ili kukamilisha taratibu za kisheria na kuwafikisha mahakamani.
Jeshi la Polisi limewataka wafugaji kuchukua tahadhari na kuhakikisha wanajenga mazizi salama kwa ajili ya kulinda mifugo yao dhidi ya vitendo vya wizi.
Aidha, Polisi limeonya kuwa litaendelea kuchukua hatua dhidi ya wafugaji wanaoacha mifugo yao ikiharibu mazao ya wakulima kwa makusudi, huku wananchi wakikumbushwa kutokujichukulia sheria mkononi.
Mwisho


