*WANAHABARI WATAKIWA KUZINGATIA TAHADHARI ZA KIUSALAMA*
Jul 5, 2026
*Na Lilian Kasenene, Morogoro**
Matukio DaimaApp
Waandishi wa habari na watangazaji wametakiwa kuzingatia tahadhari za kiusalama wanapotekeleza majukumu yao, kwa kuwa hakuna habari yenye thamani zaidi ya maisha yao.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Mussa Juma, amesema hayo Julai 4, 2026, alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu *Ulinzi na Usalama kwa Wanahabari* katika mafunzo ya wakufunzi wa wanahabari (Training of Trainers – ToT) yanayofanyika mjini Morogoro.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kusaidia Tasnia ya Habari (IMS) pamoja na JamiiAfrica, kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya. Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa *Kuwapa Nguvu Waandishi wa Habari kwa Ajili ya Jamii Zenye Taarifa*.
Juma amesema ni muhimu wanahabari kuzingatia tahadhari za kiusalama wanapotekeleza majukumu yao ili kuepuka madhara. Baadhi ya tahadhari hizo ni kutokuwa na upendeleo katika migogoro, kufanya tathmini ya usalama kabla ya kuanza kazi na kuepuka kufanya kazi wakiwa peke yao.
"Unapokwenda kuandika habari za migogoro, mikutano ya kisiasa, maandamano na matukio mengine yenye hatari, jiandae vizuri. Usiende peke yako; hakikisha una mawasiliano na mhariri wako au mwanahabari mwingine pamoja na wadau wa masuala ya haki za binadamu ili likitokea tatizo upate msaada wa haraka,"alisema Juma.
Alisema waandishi wengi waliowahi kukumbwa na madhila ya kiusalama walikuwa wakifanya kazi peke yao, walionyesha upendeleo katika migogoro au walishindwa kuzingatia tahadhari za msingi za kiusalama.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Kenneth Simbaga, aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuyathamini na kuhakikisha wanayatumia kuwajengea uwezo waandishi wengine mara watakaporejea katika maeneo yao.
"Mmepata fursa kubwa ya kushiriki mafunzo haya, lakini yanaambatana na wajibu. Nendeni mkawafundishe waandishi wengine kuhusu usalama wao binafsi, usalama wa kidijitali, ustawi wao na namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo,"alisema Simbaga.
Zaidi ya waandishi 30 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wanaowakilisha klabu mbalimbali za waandishi wa habari nchini, wanashiriki mafunzo hayo na wanatarajiwa kuwafundisha wanahabari wengine baada ya kuyakamilisha.
Mwisho.

