VETA YAWAPA NAFASI VIJANA WENYE UJUZI USIO RASMI KUPATA VYETI VYA UTAMBUZI
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendelea kuwawezesha vijana wenye ujuzi walioupata kupitia mfumo usio rasmi kwa kuwapa fursa ya kufanyiwa tathmini na kutunukiwa vyeti vinavyotambuliwa rasmi bila kulazimika kupitia mafunzo ya kawaida.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Afisa Mkuza Mtaalam Mwandamizi Veta Happiness Ladislaus Salema amesema vijana wenye ujuzi wa kazi mbalimbali wanaruhusiwa kujisajili, kufanyiwa tathmini ya uwezo wao na kupatiwa vyeti vya utambuzi hatua inayowaongezea fursa za ajira na kujiajiri.
Ameleeza kuwa zoezi hilo halihitaji vijana kulipia gharama za usajili au tathmini, likiwa na lengo la kutambua ujuzi walioupata kupitia uzoefu wa kazi na kuwapa hadhi inayotambulika katika soko la ajira.
Amesema kuwa, VETA tayari imetoa mafunzo ya ufundi stadi kwa zaidi ya vijana 20,000 nchini, ambapo kati yao 10,450 ni wanawake, kupitia vyuo mbalimbali vya VETA vilivyopo katika maeneo tofauti ya Tanzania.
Aidha, amesema taasisi hiyo inaendelea kupanua huduma zake kwa kuanzisha na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mafunzo yanazingatia mahitaji halisi ya soko la ajira na kuwafikia vijana wengi zaidi.
Hata hivyo, amesema wamenza kuandaa mfumo wa Youth Empowerment System (YES) utakaowezesha kusajili taarifa za vijana waliopata mafunzo na kuwaunganisha moja kwa moja na waajiri, taasisi za kifedha na fursa za uwezeshaji.
Ameongeza kuwa, mfumo huo utasaidia kuongeza uwazi katika utoaji wa fursa za ajira na ufadhili kwa kuondoa upendeleo, huku ukiwarahisishia waajiri kupata wahitimu wenye sifa zinazohitajika.
Msemaji huyo amebainisha kuwa hatua zinazofuata ni kuunganisha mifumo ya taarifa, kujenga kanzidata moja ya vijana waliopata mafunzo na kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali ili kuongeza ajira, ujasiriamali na maendeleo ya vijana nchini.
