TPA YAZINDUA MFUKO WA UJENZI WA MAKANISA, YAMKARIBISHA RAIS SAMIA KUCHANGIA
Jul 11, 2026
Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
CHAMA cha Maaskofu, Wachungaji, Mitume na Manabii wa Madhehebu Yote ya Kikristo Tanzania (TPA) kimezindua rasmi mfuko wa ujenzi wa makanisa na kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi kuunga mkono juhudi hizo kwa kuchangia mfuko huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Dodoma , Rais wa TPA Taifa na Askofu Mkuu wa SPCA Taifa, Dkt. Musa Mlawi, amesema TPA ni taasisi iliyoundwa kuwakutanisha maaskofu, wachungaji, mitume na manabii wa madhehebu yote ya Kikristo nchini kwa lengo la kuwa pamoja na kusaidiana katika Mambo malimbali
Ameeleza kuanzishwa kwa mfuko wa ujenzi wa makanisa ni pamoja na kufanikiwa na kuwatia moyo watumishi wa Mungu.
Amesema mfuko huo unalenga kujenga makanisa ya mijini na vijijini, hususan yale ambayo waumini wanaabudia katika maeneo yasiyo rasmi, kuwasaidia na kuwawezesha watumishi wa Mungu pamoja na viongozi wa dini kukuza huduma zao kiuchumi na kiroho, kuibua na kutatua changamoto wanazokutana nazo watumishi wa Mungu katika maeneo yao ya utumishi, kuboresha ushirikiano na Serikali katika kudumisha amani na utulivu wa nchi, pamoja na kuwahudumia wananchi bila ubaguzi wa madhehebu au dini.
Dkt. Mlawi amesema TPA haiungi mkono watu wanaohamasisha machafuko, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya taifa na kwamba ujenzi wa makanisa utasaidia kuboresha maisha ya jamii pamoja na kuimarisha maadili.
"Tunamuomba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wafadhili wa ndani na nje ya nchi, kuunga mkono na kuchangia mfuko huu ili kufanikisha malengo ya TPA," amesema Dkt. Mlawi.
Kwa upande wake, Pasta Monika Chisumuni wa Kanisa la E.A.T Ghonghona amesema chama hicho kinakuza karama na vipawa vya watumishi wa Mungu, hivyo aliwataka wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuchangia mfuko huo.
Naye Pasta Neema Lumambo wa Kanisa la Agano Jipya Ihumwa amesema makanisa mengi bado yanafanyia ibada chini ya maturubai na katika mazingira yasiyo na hadhi, hivyo ni wakati wa Watanzania kushirikiana kujenga nyumba bora za ibada.
Amesema kumtolea Mungu katika maeneo yenye uhitaji ni jambo lenye baraka na litachangia kuinua huduma za watumishi wa Mungu.
Viongozi hao pia wamesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu nchini, wakieleza kuwa uvunjifu wa amani huleta hasara kwa Serikali na wananchi wanaotegemea shughuli za kila siku kujipatia kipato.
Wamesema baada ya uchaguzi ni wakati wa Watanzania kuendelea kushirikiana katika kujenga taifa lenye umoja na maendeleo.
Aidha, Dkt. Mlawi alisema wadau wanaotaka kuunga mkono mfuko huo wanaweza kutuma michango kupitia akaunti ya NMB namba 51110029407, Airtel Money namba 0784 805 863 na M-Pesa namba 0762 422 121, akisisitiza kuwa mchango huo hauna ubaguzi wa dhehebu wala dini bali ni kwa mtu yeyote mwenye nia ya kuunga mkono malengo ya TPA.
Mwisho


