*TANZANIA KUPITIA ATCL YAENDELEA KUJITANUA KIMATAIFA.
Jul 3, 2026
📍YAZINDUA SAFARI ZA MOJA KWA MOJA DAR ES SALAAM–MOSCOW KUCHOCHEA ONGEZEKO LA WATALII.
TANZANIA, kupitia Shirika lake la ndege imezindua rasmi safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Jiji la Moscow nchini Urusi.
Uzinduzi wa safari hizo umefanyika hii leo katika Jiji la Moscow nchini Urusi ikiwa ni jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kufungua na kuimarisha sekta ya Utalii nchini.
Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) imetua katika Jiji la Moscow kwa mara ya kwanza ikitokea Dar es Salaam ikiwa na ujumbe kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ulioongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, baadhi ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na viongozi mbalimbali wa wizara na mawakala wa utalii kutoka Tanzania.
Akizungumza jijini Moscow, Dkt. Kijaji alisema kuanza kwa safari hizo za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Moscow inatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watalii wa kimataifa wanaotembelea Tanzania.
Alisema kwa muda mrefu watalii wengi kutoka nje ya nchi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa safari za moja kwa moja kwenda Tanzania, na kwamba uzinduzi wa safari hiyo ni fursa muhimu kwa maendeleo ya Sekta ya Utalii.
Dkt. Kijaji ameongeza kuwa Tanzania inatarajia kupokea ongezeko kubwa la watalii kutoka Urusi pamoja na nchi jirani.
"Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Utalii ya Urusi, Tanzania ilikuwa inapokea watalii takribani 17,100 kutoka Urusi. Hata hivyo, kutokana na kuanza kwa safari za moja kwa moja, matarajio yetu ni kupokea zaidi ya watalii 200,000." Alisema Dkt. Kijaji
"Tunamshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake na uzalendo mkubwa kwa nchi yetu. Uzinduzi huu ni matokeo chanya ya filamu za The Royal Tour na Amazing Tanzania," alisema.
Aliongeza kuwa kupitia filamu hizo, Tanzania imeendelea kuvutia watalii wengi kutoka nchi za Ulaya, Marekani, pamoja na nchi za Mashariki ya Mbali.
Dkt. Kijaji alisema ujumbe wa Tanzania uliowasili nchini Urusi umeambatana na mawakala kutoka Kampuni 47 za Utalii nchini ambao watakutana na mawakala zaidi ya 92 kutoka Kampuni za Utalii nchini Urusi.
"Licha ya mawakala hawa wa Tanzania kupata fursa ya kukutana na wenzao wa Urusi, tunatarajia pia kufanya Kongamano Maalumu ndani ya miezi miwili ijayo litakalowakutanisha mawakala wengi zaidi wa utalii kutoka Tanzania na Urusi," aliongeza.
Waziri Kijaji alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano na Urusi ili kuhakikisha watalii wengi zaidi wanapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.
"Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza takribani shilingi bilioni 300 katika kuboresha miundombinu ya utalii katika Kanda ya Kusini. Hatua hiyo imewezesha ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege vinavyohudumia maeneo ya Hifadhi za Mikumi, Ngerengere na Ruaha," alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alisema uzinduzi wa safari hizo ni fursa ya kipekee kwa Tanzania, kwani pamoja na kurahisisha usafiri kati ya Tanzania na Urusi, utachangia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta ya utalii na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Aidha, ndege ya ATCL itakuwa ikifanya safari zake mara tatu kwa wiki kati ya Dar es Salaam, Zanzibar na Moscow, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za biashara, uwekezaji na usafiri wa watalii pamoja na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi.





