Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
POLISI KATA ATOA MADAWATI 10 KUPUNGUZA KERO SHULE YA MSINGI MATOMBO

POLISI KATA ATOA MADAWATI 10 KUPUNGUZA KERO SHULE YA MSINGI MATOMBO

 

Na Matukio Daima Media, Morogoro

POLISI Kata wa Konde, Tarafa ya Matombo, Wilaya ya Morogoro, Inspekta Edith Msafiri, ametoa madawati 10 kwa Shule ya Msingi Matombo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati unaowakabili wanafunzi wa shule hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo mbele ya viongozi wa elimu na uongozi wa shule, Msafiri amesema ameamua kuchangia katika kuboresha mazingira ya kujifunzia baada ya kuguswa na hali ya wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini kutokana na ukosefu wa madawati.

Amesema licha ya kuwa askari polisi, yeye pia ni mzazi na ana wajibu wa kushiriki katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii, hususan zinazohusu elimu ya watoto.

Kwa mujibu wa Msafiri, madawati hayo yaliyopatikana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali yatawanufaisha zaidi ya wanafunzi 30, hivyo kuwapa mazingira bora ya kusoma na kuongeza hamasa ya kuhudhuria shule.

Akikabidhi madawati hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Afisa Elimu wa Halmashauri hiyo, Gideon Bunto, ameishukuru Serikali kwa kujenga uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, akisema hatua hiyo imewezesha askari kushiriki moja kwa moja katika shughuli za maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Matombo, Mohamed Rarabu, amesema pamoja na msaada huo, shule hiyo bado inakabiliwa na upungufu wa madawati 321, hivyo kuomba wadau wengine kujitokeza kushirikiana na shule hiyo katika kumaliza changamoto hiyo.

Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3