MZANI JANJA WAONDOA KILIO CHA WAKULIMA WA ZAO LA PAMBA
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA.
Kilio cha muda mrefu cha wakulima wa pamba kuhusu udanganyifu wa vipimo na makato yasiyo halali kinaendelea kupungua baada ya Serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania kuanzisha matumizi ya mizani janja, teknolojia inayotajwa kurejesha uwazi na haki katika ununuzi wa zao hilo.
Afisa Kilimo wa Bodi ya Pamba Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, Hamed Kabeya, amesema mizani janja ilianzishwa kufuatia changamoto zilizokuwa zikijitokeza kwenye mizani ya analogia, ambapo baadhi ya watu walikuwa na uwezo wa kuichezea bila mkulima kugundua na hivyo kuathiri mapato yake.
"Kipindi cha nyuma kulikuwa na mizani ya analogia na mtu yeyote alikuwa na uweza wa kufanya chochote, na mkulima asigundea kama kuna kitu kimefanyika, lakini sasa mkulima anapewa risiti ya kielektroniki na anaona kilo halisi alizopimiwa" amesema Kabeya.
Ameongeza kuwa licha ya msimu uliopita baadhi ya watu kujaribu kuchezea mfumo huo kwa maslahi yao binafsi, walichukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu, huku maboresho zaidi yakifanyika ambapo mzani hujizima endapo utachezewa.
"Kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya wa Meatu tuliwaelekeza viongozi wa AMCOS kuwa mtu yeyote atakayeharibu au kuchezea mzani, hata kama ni mwenzetu, atachukuliwa hatua kwa sababu anahujumu haki za wakulima," amesema Kabeya.
Kabeya amesema mizani hiyo imeunganishwa na printer na simu maalumu inayowezesha kutoa risiti halali ya kielektroniki, huku wakulima wote wakisajiliwa kwenye mfumo wa kidijitali ili kuhakikisha takwimu sahihi za wazalishaji zinapatikana.
"Tulitoa mafunzo kwa wenyeviti na makatibu wa AMCOS namna ya kutumia mizani janja, leo mkulima anauza pamba akiwa na uhakika wa kilo zake na anaondoka na risiti yake halali, jambo lililoondoa malalamiko yaliyokuwepo zamani," amesema Kabeya.
Aidha amesema Wilaya ya Meatu yenye kata 29 imelima takribani ekari 153,000 za pamba kwa msimu wa 2025/2026 na inatarajia kuvuna kati ya kilo milioni 44 mpaka milioni 45.
Katibu wa AMCOS Nkoma, Anthony Machibya, amesema viongozi wa vyama vya msingi walipatiwa mafunzo ya matumizi ya mizani janja na baadaye kuwapa elimu wakulima kuhusu mfumo huo pamoja na matumizi ya vifungashio vinavyokidhi viwango.
"Wakulima wameipokea teknolojia hii kwa furaha. Changamoto iliyobaki ni baadhi yao kutumia vifungashio vizito badala ya vile vinavyotakiwa, lakini tunaendelea kutoa elimu," amesema Machibya.
Kwa upande wake, Meneja wa Chama cha Msingi cha AMCOS Mwanhuzi, Daniel Sayi, amesema tofauti kubwa ya mizani janja na mizani ya zamani ni kwamba mkulima analipwa kilo zote alizovuna bila kukatwa hata kilo moja kwa madai ya uchafu au kifungashio.
"Kwa sasa mkulima analipwa kilo zote hadi nukta alizopata, hakuna tena lawama kuwa ameibiwa kwa sababu mfumo unatoa kilo halisi na malipo halisi, Kuna mkulima alipima pamba nyumbani, alipofika ghalani akakuta zimeongezeka kilo tisa, jambo lililoimarisha imani ya wakulima," amesema.
Wakulima wa zao la pamba wameeleza kuwa matumizi ya mizani hiyo yamewarejeshea matumaini na kuondoa hofu ya kupunjwa wakati wa kuuza mazao yao.
Mkulima wa Kijiji cha Nkoma, Mandago Charles Nzengo, amesema tofauti za vipimo zilizokuwa zikijitokeza zamani zimeondoka.
"Sasa tunapima pamba nyumbani na tukifika ghalani tunapata uzito ule ule. Serikali imetuletea mfumo mzuri unaotupa haki yetu," amesema.
Naye mkulima wa Kata ya Mwanhuzi, Taliguli Mambo, amesema kuondolewa kwa makato ya kilo moja kwa ajili ya kifungashio kumewapa motisha wakulima wengi kuendelea kulima pamba, ingawa bado wameiomba Serikali kuboresha bei ya zao hilo.
"Zamani kwenye kilo hamsini ni lazima ukatwe kilo moja kwa ajili ya kifungashio, Sasa hilo limeondoka na limetupa moyo wa kuendelea kulima pamba, ingawa tunaomba bei ya pamba iongezwe," amesema.
Kwa upande wake, mkulima Mkulima kutoka Mwanhuzi Mabere Mathias amesema mwanzoni baadhi ya wakulima waliiona teknolojia hiyo kuwa ngeni, lakini elimu waliyopewa imewasaidia kuielewa na kuikubali.
"Mwaka jana ilikuwa mizani hiyo ilipoletwa wakulima wengi waliona ni kitu kipya na wengi walikuwa hawaielewi, lakini baada ya kupewa elimu sasa tunaona faida zake na wakulima wengi wameikubali," amesema.
Matumizi ya mizani janja sasa yanatajwa kuwa yameongeza uwazi, uaminifu na haki katika biashara ya pamba, hatua inayorejesha imani ya wakulima na kuwapa motisha ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo.


