LIVERPOOL YAANDAA OFA YA KWANZA KUMSAJILI BARCOLA KUTOKA PSG
Liverpool imeongeza juhudi zake za kumsajili winga wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola, na inajiandaa kuwasilisha ofa yake ya kwanza kwa klabu hiyo ya Ufaransa.
Barcola, mwenye umri wa miaka 23, ametajwa kuwa chaguo kuu la Liverpool katika harakati za kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mohamed Salah, aliyeondoka mwishoni mwa msimu uliopita.
PSG inasema thamani ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa ni pauni milioni 145.
Iwapo usajili huo utakamilika kwa kiasi hicho, utavunja rekodi ya uhamisho ghali zaidi kuwahi kufanyika nchini Uingereza. Hata hivyo, viongozi wa Liverpool wana matumaini ya kufikia makubaliano kwa ada inayokaribia pauni milioni 100.
Barcola amebakiza miaka miwili katika mkataba wake na PSG, lakini inaelezwa kuwa yuko tayari kuhamia Liverpool akitafuta changamoto mpya, baada ya nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Ufaransa kupungua.
Awali, Liverpool ilikuwa ikimwania winga wa RB Leipzig Yan Diomande, lakini sasa mchezaji huyo anatarajiwa kujiunga na Real Madrid.
Barcola alikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichofika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia la 2026.