TAKUKURU MBEYA YAREJESHA MALI ZA SHILINGI MILIONI 150 ZA KIKUNDI CHA ASANTE MBEYA PROJECT
Na: Samwel Mpogole-Mbeya.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya imefanikiwa kurejesha mali zenye thamani ya takribani shilingi milioni 150 zakikundi cha Asante Mbeya Project baada ya kubaini jaribio la mwanzilishi wa kikundi hicho kujimilikisha kwakificho.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Jasper Luoga, amesema mali hizo ni pamoja na magari matatu na vifaa mbalimbali vya matumizi ya kikundi hicho.
Amefafanua kuwa magari yaliyorejeshwa ni mabasi mawili aina ya Toyota Coaster yenye namba za usajili T475 EJF na T233 EJF pamoja na gari moja aina ya Toyota LiteAce Noah. Aidha, vifaa vya chakula vilivyonunuliwa kwa michango ya wanachama wa kikundi hicho navyo vimerejeshwa.
Kwa mujibu wa Luoga, uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU ulibaini kuwa mali hizo zilinunuliwa kupitia michango ya wanachama wa Asante Mbeya Project pamoja na mwanzilishi wa kikundi hicho, Daniel Mwanakatwe, ambaye alidaiwa kuwa na nia ya kuwadhulumu wanachama wengine kwa kuzimiliki mali hizo isivyo halali.
"TAKUKURU ilifanya uchunguzi wa kina na kufanikiwa kurejesha mali zote kwa manufaa ya wanachama wa kikundi hicho, hatua inayolenga kulinda haki na maslahi ya wananchi," amesema Luoga.
Katika hatua nyingine, Luoga amesema TAKUKURU Mkoa wa Mbeya imefungua majalada mawili ya uchunguzi yanayohusisha miradi ya maendeleo baada ya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi hiyo kubaini kuwepo kwa mapungufu makubwa.
Amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha kasoro hizo na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kuhusika na ubadhirifu au matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma.
TAKUKURU imeeleza kuwa itaendelea kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za umma na kushirikiana na wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa na vitendo vyote vinavyohujumu maendeleo ya jamii.
.jpeg)

