ONYO KWA BIASHARA HARAMU YA BINADAMU
Jun 30, 2026
Na MatukioDaima, Singida,
Jumanne juni 30,2026.
Biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu imeendelea kuwa tishio kwa vijana, hasa wasichana wanaorubuniwa kwa ahadi za ajira na maisha bora nje ya nchi. Kutokana na hali hiyo, viongozi wa dini, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa serikali za mitaa wametakiwa kushirikiana ili kukomesha uhalifu huo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la CARITAS mjini Singida, Padre Simon Gwanoga amesema kuwa wahalifu hao hutumia mbinu mbalimbali kuwarubuni waathirika, lakini wanapowafikisha ugenini huwanyang'anya hati za kusafiria na kuwalazimisha kufanya shughuli za kipuuzi na za kinyonyaji.
Aidha mwanasheria Sista Stellah Martin amesema biashara hiyo ni kosa kubwa la jinai na ukiukwaji wa haki za binadamu, akibainisha kuwa matumizi mabaya ya teknolojia yamechangia kuongezeka kwa matukio hayo katika mataifa mbalimbali duniani.
Mratibu wa CARITAS Mkoa wa Singida, Baptista Mameho, ametaka wananchi kushiriki kutoa elimu na taarifa sahihi kwa mamlaka husika ili kuwalinda watoto na vijana dhidi ya walanguzi wa binadamu, huku baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakitaja umasikini na ukosefu wa elimu kwamba ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya tatizo hilo.



