Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MWANASHERIA WA KENYA MARTHA KARUA AZUIWA KUINGIA UGANDA - SHIRIKA LA MAWAKILI

MWANASHERIA WA KENYA MARTHA KARUA AZUIWA KUINGIA UGANDA - SHIRIKA LA MAWAKILI

 

Wakili mkuu wa Kenya na Waziri wa Sheria wa zamani Martha Karua amezuiwa kuingia Uganda na kuamriwa kurejea nyumbani, kulingana na Chama cha Wanasheria cha Uganda.

Karua alikuwa amewasili tu katika uwanja wa ndege wa Entebbe kuungana na timu inayomtetea wakili mwenzake kutoka Uganda Erias Lukwago, ambaye wamekuwa wakimwakilisha kiongozi wa upinzani aliyezuiliwa Kizza Besigye, anayekabiliwa na kesi ya uhaini.

Lukwago mwenyewe alishtakiwa wiki iliyopita kwa kosa linalohusiana na uhaini, na kesi yake ya kusikilizwa ombi la dhamana ilikuwa imepangwa kufanyika leo Jumatatu.

Taarifa kutoka ofisi yake ya utendaji inasema kuwa tangu alipowasili Entebbe asubuhi ya leo, Karua hajaweza kupatikana kwa mawasiliano, simu zake za mkononi zimezimwa na hakuna mawasiliano ya moja kwa moja yaliyopokelewa kuhusu alipo au hali yake.

“Karua alikuwa amepangiwa kurejea Nairobi leo lakini bado hajapatikana kwa mawasiliano,” taarifa hiyo inasema.

Kwa mujibu wa ofisi yake, aliwasili Entebbe asubuhi hii kwa ndege ya Kenya Airways akiwa pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Kenya, Charles Kanjama.

Wawili hao walikuwa wakisafiri kuhudhuria uamuzi wa mahakama kuhusu ombi la kuachiliwa kwa dhamana la mwanasheria na meya wa zamani wa Jiji la Kampala, Erias Lukwago, ambaye anakabiliwa na shtaka linalohusiana na uhaini.

Wakati Bw. Kanjama aliruhusiwa kuingia nchini, Bi. Karua anaripotiwa kuzuiliwa mara tu alipowasili katika uwanja wa ndege. Kwa mujibu wa Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki, anatarajiwa kurejea Nairobi baadaye leo.

Timu yake ya wanasheria imeeleza wasiwasi kuhusu hali yake ya kutowasiliana na mtu yeyote na kusema kuwa inatafuta ufafanuzi kutoka kwa mamlaka za Uganda.

Mamlaka za Uganda bado hazijatoa taarifa yoyote kuhusu sababu za kuzuiliwa kwake au kunyimwa ruhusa ya kuingia nchini.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3