FURSA MPYA ZA MASOMO URUSI KUNUFAISHA WATANZANIA
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
TANZANIA inatarajia kunufaika na fursa zaidi za elimu ya juu, tafiti na maendeleo ya teknolojia kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tanzania na Urusi wakati wa ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini humo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema makubaliano hayo yamefungua njia mpya za ushirikiano wa kitaaluma kati ya taasisi za elimu za nchi hizo mbili, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa Watanzania katika nyanja mbalimbali za elimu na utafiti.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Prof. Mkenda alisema moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni kupatikana kwa nafasi 10 za ufadhili wa masomo kutoka Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN), ambazo zitawanufaisha wanafunzi wa Kitanzania watakaokidhi vigezo.
Amesema pamoja na ufadhili huo, Tanzania na Urusi zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kubadilishana wanafunzi, wahadhiri na wataalamu ili kuongeza ubora wa elimu na kukuza tafiti zenye tija kwa maendeleo ya mataifa hayo.
"Makubaliano hayo pia yatawezesha kuimarishwa kwa ufundishaji wa lugha za Kiswahili na Kirusi, hatua itakayorahisisha mawasiliano na ushirikiano wa kitaaluma kati ya pande hizo mbili, " Amesema Prof. Mkenda,
Katika utekelezaji wa ushirikiano huo, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeingia makubaliano yatakayowapa wanafunzi fursa ya kusoma katika vyuo vya Tanzania na Urusi kwa mfumo wa pamoja, unaotarajiwa kuongeza maarifa na uzoefu wa kimataifa kwa wahitimu.
Amesema Serikali inaendelea kukamilisha taratibu za utambuzi wa vyeti na sifa za kitaaluma kati ya nchi hizo ili kuweka mazingira rafiki kwa wahitimu wanaotaka kufanya kazi au kuendelea na masomo katika nchi husika.
Prof. Mkenda amesema Serikali itaendelea kuhamasisha vijana kutumia fursa zinazopatikana kupitia ushirikiano wa kimataifa, hususan katika maeneo ya sayansi, teknolojia na uhandisi ambayo yana mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa taifa.


