Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
FUNDI MCHINA AKAMATWA TUHUMA ZA KUSHAMBULIA WAFANYAKAZI MORO

FUNDI MCHINA AKAMATWA TUHUMA ZA KUSHAMBULIA WAFANYAKAZI MORO

 


Matukio Daima, Morogoro 


JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia Zhou Zhi (36), Fundi Minara wa Kampuni ya kusambaza umeme wa REA iitwayo TBEA, raia wa China, kwa tuhuma za kuwashambulia wafanyakazi wawili wa kampuni hiyo.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amesema tukio hilo limetokea Juni 19, 2026 katika Kitongoji cha Sokoine Ranch, Kijiji cha Wami Sokoine, Kata ya Dakawa, Wilaya ya Mvomero.


Kwa mujibu wa Kamanda huyo, Zhou Zhi anadaiwa kutekeleza tukio hilo kwa kushirikiana na wenzake ambapo wamewashambulia Stephen Athuman Mwampaka (44), dereva wa kampuni hiyo na mkazi wa Sokoine, pamoja na Mbaraka Selemani Ally (18), ambaye ni kibarua wa kampuni hiyo.


Amesema waathirika hao walipata majeraha baada ya kupigwa katika sehemu mbalimbali za miili yao kwa kutumia kitu butu.


ACP Kantimbo amesema mtuhumiwa huyo anaendelea kushikiliwa katika Kituo cha Polisi Mvomero wakati uchunguzi wa shauri hilo ukiendelea kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.


Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kumtafuta Yung Lu, ambaye ametajwa kuhusishwa na tukio hilo na bado hajatiwa nguvuni.


Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limefafanua taarifa zinazozunguka katika mitandao ya kijamii kuhusu Japhary Saidi Kahise.


ACP Kantimbo amesema Juni 5, 2026, katika operesheni maalumu ya kuzuia na kutanzua uhalifu iliyofanyika eneo la Kihonda, Manispaa ya Morogoro, walikamatwa Exavery Abdulmajid Yusuph (20), Japhary Saidi Kahise (23) na Fadhili Shedrack Nyambalo (19).


Amesema watuhumiwa hao walikuwa wakifuatiliwa kutokana na kuhusishwa na matukio mbalimbali ya kihalifu yaliyokuwa yakiripotiwa ndani ya Mkoa wa Morogoro.


Miongoni mwa tuhuma zinazowakabili ni uporaji wa simu katika maeneo tofauti ya mkoa huo, unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na wizi wa pikipiki ulioripotiwa kutokea Wilaya ya Mvomero, huku uchunguzi zaidi ukiendelea.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3