Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
ATCL YATANGAZA SAFARI MPYA AFRIKA

ATCL YATANGAZA SAFARI MPYA AFRIKA

 


Na Matukio DaimaMedia 


Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imeendelea kupanua mtandao wake wa safari za ndani na kimataifa kwa kutangaza mipango ya kufungua njia mpya za ndege katika bara la Afrika, hatua inayolenga kuimarisha biashara, utalii na uwekezaji.

‎Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Juni 26, Mkurugenzi wa Biashara wa ATCL, Dominic Louis, alisema kampuni hiyo inakamilisha maandalizi ya kiufundi na kibiashara kwa ajili ya kuanzisha safari mpya kuelekea Maputo na Nampula nchini Msumbiji, Dakar nchini Senegal, Abidjan nchini Ivory Coast pamoja na Juba nchini Sudan Kusini.

‎Alisema kufunguliwa kwa safari hizo kutaimarisha uunganishaji wa Tanzania na masoko mapya ya Afrika, huku zikichochea ukuaji wa biashara, utalii na fursa za uwekezaji.

‎"Kufunguliwa kwa safari hizi kutasaidia kuongeza uunganishaji wa Tanzania na masoko mapya pamoja na kukuza biashara, utalii na uwekezaji," alisema Louis.

‎Mbali na safari hizo mpya, Louis alisema ATCL tayari imeanza safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Ushelisheli kuanzia Juni 2026, ambapo safari hizo hufanyika kila Jumatano, Ijumaa na Jumapili.

‎Aidha, alisema kuanzia Julai 1, 2026, kampuni hiyo itaanza safari za moja kwa moja kwenda Moscow nchini Urusi kwa miruko mitatu kwa wiki, ambayo ni Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.

‎ATCL pia inaendelea na maandalizi ya kuanzisha safari za moja kwa moja kuelekea Muscat nchini Oman, huku ikiongeza idadi ya safari kati ya Dar es Salaam na Mumbai, India kutoka safari nne kwa wiki hadi safari za kila siku ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya wasafiri.

‎Kwa upande wa safari za ndani, Kaimu Meneja Mawasiliano wa ATCL, Jerry Ngewe, alisema safari za abiria kuelekea Shinyanga zitaanza rasmi Septemba 2026 baada ya kukamilika kwa majaribio ya kupaa na kutua yaliyofanyika hivi karibuni.

‎Ngewe aliongeza kuwa kampuni hiyo pia imeongeza miruko miwili katika baadhi ya njia za ndani ikiwemo Dar es Salaam–Geita–Mwanza, Dar es Salaam–Kilimanjaro–Mwanza, Dodoma–Mwanza pamoja na Dar es Salaam–Sumbawanga–Tabora.

‎Hatua hiyo inaonesha dhamira ya ATCL ya kuendelea kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini kwa kuongeza idadi ya safari, kufungua masoko mapya ya kimataifa na kuimarisha mtandao wa usafiri wa ndani kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa taifa.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3