WCF MBIONI KUSAJILI SEKTA ISIYOKUWA RASMI KUPATA FAO LA FIDIA ZA MAJANGA
NA ARODIA PETER
MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) upo mbioni kuanza kuwatambua na kuwasajili Watanzania waliojili katika sekta isiyo rasmi, lengo likiwa ni kuwapunguzia adha za majanga ya kutumia, kuugua ama kufariki dunia kutokana na kazi wanazozifanya.
Hayo yamebainishwa na Afisa Matekelezo wa WCF, Ayoub Bendera wakati wa kikao kazi cha Wafanyakazi wa vyombo vya habari Tanzania (JOWUTA) pamoja na mfuko huo kikichofanyika Dar es Salaam, Mei 25,2026.
Bendera alisema, moja ya mikakati ya muda mrefu ya WCF ni kuhakikisha sekta isiyo rasmi nayo inanufaika na mafao ya mfuko huo wao binafsi pamoja na wategemezi wao.
Alisema, Sheria iliyounda mfuko huo ilikuwa na lengo la kuhudumia wafanyakazi wa waliopo sekta ya umma na binafsi endapo watakumbana na majanga ya kuumia, kuugua, ama kufariki dunia kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba yao.
Bendera alitolea mfano, wafanyakazi waliopo kwenye sekta isiyo rasmi upande wa madini, ambapo alisema kulingana na asili ya kazi hizo Kuna umuhimu mkubwa kuandikishwa na kujiunga na WCF.
"Hata hivyo, huu ni moja ya mkakati wa muda mrefu wa serikali kupitia WCF kuhakikisha huduma hizi zinawafikia watu wanaofanyakazi kwenye sekta isiyo rasmi linafanyiwa tathimini na kufikia muafaka wake" alisema Bendera.
Kuhusu mafao yatolewayo na WCF, Afisa Madai wa mfuko huo alieleza kuwa mfanyakazi aliyesajiliwa anaanza kupata huduma za matibabu saa chache baada ya kuumia na kuendelea hadi miezi 24 kutokana na aina ya ugonjwa husika.
"Huduma hiyo ya matibabu itahusisha gari maalum la kusafirisha wagonjwa (ambulance), kumuona daktari, vipimo vya uchunguzi, upasuaji, huduma za uuguzi, dawa, kurudia matibabu itakapobidi pamoja na viungo bandia.
"Kuhusu fidia ya ulemavu, fao hili hulipwa kwa mfanyakazi aliyepata ajali au ugonjwa unakoelekea kulazwa, kupatiwa siku ya mapumziko ya kujiuguza zaidi ya siku tatu au kazi nyepesi. Ambapo fao hili hulipwa kwa kipindi kisichozidi miezi 24 toka ilipotokea ajali au kugundulika kwa ugonjwa." alisema Temu.
Aidha kikao kazi hicho kilifunguliwa na Rais wa TUCTA, ...Nyamuhokya ambaye aliwasihi wana habari kuulinda mfuko huuo kutokana na umuhimu wake kwa taifa.
"Mafao yatolewayo na mfuko huu ni mengi lakini muhimu zaidi mafao haya yananufaisha pia wategemezi wa mfanyakazi endapo atafariki dunia kutokana na kazi zake. Ndiyo maana nawaambia WCF ni taasisi yetu, hivyo tuna wajibu kuilinda kwa nguvu zetu zote kuhakikisha inakuwa himilivu" alisema Nyamuhokya.




