WAZIRI ULEGA ATAKA MAENEO SALAMA YA KUVUKA BARABARA DODOMA
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewataka wataalamu na wasanifu wa mradi wa upanuzi wa barabara ya njia sita kutoka Dodoma CBD hadi Chamwino kuzingatia masuala ya usalama kwa kuweka maeneo salama ya kuvuka barabara ili kupunguza ajali zinazoweza kujitokeza katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Ulega ametoa maelekezo hayo leo Mei 18, 2026 wakati akishuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 32 katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Mashujaa jijini Dodoma.
Mradi huo utakaotekelezwa kwa gharama ya takribani Sh bilioni 241, umesainiwa kati ya TANROADS kwa niaba ya Serikali na kampuni ya China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) ya China kwa lengo la kupanua barabara hiyo kuwa ya njia sita.
Katika maelekezo yake, Ulega amesema barabara hiyo inapaswa kuwa na taa za kisasa za barabarani, bustani, njia za watembea kwa miguu pamoja na miundombinu ya kisasa itakayolifanya Jiji la Dodoma kuvutia zaidi.
“Tunataka mtu akipita usiku aione Dodoma inavyong’ara taa za barabarani lazima ziwe za viwango vya juu,” amesema Ulega.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya miundombinu kupitia ujenzi wa barabara na madaraja kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za usafiri nchini.
Ameeleza kuwa sambamba na mradi huo, Serikali tayari imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa ndani wa Jiji la Dodoma yenye urefu wa kilometa 6.4 inayofadhiliwa na Serikali ya Japan kwa gharama ya yen bilioni 2.78
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mohamed Besta, amesema mradi huo utatekelezwa kwa utaratibu wa Sanifu na Jenga (Design and Build) na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36 ikiwemo miezi sita ya usanifu pamoja na miezi mitatu ya maandalizi ya awali.





