Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WAKAZI WA TANGA WAMPAGAWISHA KAMANDA ZIMAMOTO.

WAKAZI WA TANGA WAMPAGAWISHA KAMANDA ZIMAMOTO.

 

Na Amina  Saidi,

Matukio Daima Media Tanga.

JESHI la Zima Moto na Uokoaji mkoani Tanga limeeleza kusikitishwa na tabia inayozidi kushamiri ya baadhi ya wananchi mkoani humo, wanaotumia namba ya dharura ya jeshi hilo (114) kuomba gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) badala ya huduma za zimamoto na uokoaji.

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tanga, Mrakibu Mwandamizi Katala Issa,wakati  akizungumza na mwandishi wa Matukio Daima Amina Saidi  ofisini kwake,


Kamanda Issa amefafanua kuwa hali hiyo inasababisha usumbufu mkubwa na kuingilia utendaji kazi wa jeshi hilo ambao unalenga kuokoa maisha ya watu na mali zao kwa haraka.

​Akifafanua kuhusu mkanganyiko huo, Kamanda Issa amesema kuwa Jeshi la Zimamoto mkoani Tanga linamiliki gari maalumu la huduma ya kwanza na kubebea majeruhi (Rescue Ambulance), Hata hivyo amesisitiza kuwa gari hilo limetengenezwa maalumu kwa ajili ya kuwahudumia na kuwabeba majeruhi wanaotokana na matukio ya moto na uokoaji pekee, na si kwa ajili ya wagonjwa wa kawaida wa majumbani au mahospitalini.

​"Ni kweli tunalo gari maalumu na la kisasa kwa ajili ya kutoa huduma ya kitabibu na uokoaji, lakini gari hili limekusudiwa kuhudumia majeruhi waliokolewa kwenye janga la moto au ajali tunazozishughulikia Kumekuwa na changamoto ya wananchi kutupigia simu wakitaka gari hili liwapeleke wagonjwa wao hospitalini, jambo linaloleta usumbufu," alieleza Kamanda Issa.

​Kamanda Issa ametoa rai nzito kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga kuacha mara moja tabia hiyo, Amebainisha kuwa wananchi wanapohitaji huduma za kitabibu kwa wagonjwa wa kawaida, wanapaswa kuwasiliana moja kwa moja na mamlaka za afya au kupiga namba za magari ya dharura ya kubebea wagonjwa (Ambulance) za hospitalini, na sio kutumia namba 114.


​Jeshi hilo limebainisha kuwa matumizi yasiyo sahihi ya namba ya dharura ya 114 yanahatarisha usalama wa jamii inapotokea mwananchi ameshikilia laini ya dharura kwa ajili ya kuomba gari la wagonjwa, anakuwa anazuia nafasi kwa mtu mwingine mwenye janga la moto au dharura ya uokoaji anayehitaji msaada wa haraka wa kuzima moto.


 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Tanga limejipanga kuanza kampeni maalumu ya kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara, Lengo likiwa ni kuwajengea wananchi uelewa wa utofauti kati ya magari ya zimamoto na yale ya huduma za afya, ili kuondoa usumbufu huo uliopo sasa.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3