WAFANYABIASHARA IGUMBILO WAMLILIA WAZIRI MKUU MABASI KUTOINGIA STENDI
Na Matukio Daima Media , Iringa
WAFANYABIASHARA wadogo wanaofanya biashara katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Mikoani ya Igumbilo mjini Iringa wamemuomba Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, kuingilia kati mgogoro wa mabasi kutotumia stendi hiyo hali inayodaiwa kudororesha biashara zao.
Walisema wenye mabasi wamekuwa hawaingii stendi hiyo kwa zaidi ya wiki moja sasa na sababu kubwa wanadai serikali iliwaruhusu kama hakuna abiria wa kupanda ama kushuka stendi hakuna haja ya basi kuingia stendi .
Hivyo kutokana na kauli hiyo wenye mabasi wamechukulia kama kinga ya wao kutoingia kabisa stendi na hivyo kupelekea shughuli za kibiashara maeneo ya stendi kukosa wateja .
Wakizungumza na Matukio Daima jana katika stendi hiyo, wafanyabiashara hao walieleza kuwa hali ya biashara imekuwa ngumu kutokana na mabasi mengi kupita bila kuingia stendi, huku mengine yakiingia lakini abiria kushuka wakiwa tayari wameshahudumiwa njiani.
Mfanyabiashara mmoja, Julieth Togera, alisema awali biashara ilikuwa nzuri wakati stendi hiyo ilipoanza kutumika, lakini sasa hali imekuwa mbaya kutokana na kuwepo kwa stendi nyingi zinazotumiwa na mabasi, jambo ambalo limechangia kupungua kwa wateja.
Alisema hali hiyo imewaathiri kiuchumi na kuhatarisha mitaji yao, huku wakikabiliwa na majukumu ya kifamilia ikiwemo kulipia ada za watoto na mahitaji mengine ya msingi.
“Tunaomba serikali itoe maelekezo ya wazi kuhusu stendi rasmi ya mabasi ya mikoani kati ya Mlandege, Ipogolo, Kihesa na Igumbilo, kwani hali ya sasa inatuchanganya na kutuathiri sisi wafanyabiashara,” alisema Togera.
Kwa upande wake, Mariam Kapinga alisema kwa zaidi ya wiki mbili sasa mabasi mengi hayajaingia stendi hiyo, hali inayosababisha bidhaa zao kuharibika kutokana na kukosa wateja.
Alisema yeye huuza machungwa ambayo hulazimika kuyamenya na kukaa nayo juani siku nzima bila kupata wanunuzi, jambo linalomlazimu kula sehemu ya bidhaa hizo na watoto wake ili zisiharibike kabisa.
“Hali ni ngumu sana. Mitaji yetu inaendelea kuyeyuka huku maisha yakizidi kuwa magumu kila siku,” alisema Kapinga.
Afisa usafirishaji katika eneo hilo, Saidi Jumanne, alisema hali ya shughuli za usafirishaji katika stendi hiyo imezorota kwa kiasi kikubwa kutokana na mabasi mengi kupitiliza bila kuingia stendi.
Alidai baadhi ya maeneo ya barabarani yamegeuzwa vituo vya kupakia na kushusha abiria, hali inayosababisha stendi hiyo kupoteza umuhimu wake.
“Kutokana na hali hii, baadhi ya maafisa usafirishaji wameacha kazi na mama lishe wengi wamefunga biashara zao kwa kukosa wateja,” alisema Jumanne.
Wafanyabiashara hao wameiomba serikali kuingilia kati haraka ili kurejesha matumizi rasmi ya stendi hiyo na kuokoa biashara pamoja na ajira zinazotegemea shughuli za usafirishaji.Hata hivyo mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada hakuweza kupatikana kueleza mkakati wa Halmashauri hiyo kwa stendi ya Igumbilo kiuchumi
TAZAMA VIDEO BOFYA LINK HII








