Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TGNP YASHIRIKIANA NA WADAU KUSUKUMA BAJETI YA AFUA ZA ULINZI WA MTOTO

TGNP YASHIRIKIANA NA WADAU KUSUKUMA BAJETI YA AFUA ZA ULINZI WA MTOTO

 


Na Deogratius Temba, Dodoma

Wadau kutoka asasi za kiraia wanaotekeleza afua za ulinzi wa mtoto wameitaka Serikali kuongeza uwekezaji wa ndani katika afua za haki na ulinzi wa mtoto kupitia upangaji wa bajeti kwa kuzingatia misingi ya Bajeti yenye Mrengo wa kijinsia (GRB), ili kuhakikisha huduma hizo zinakuwa endelevu na zenye matokeo chanya kwa watoto wa kike na wa kiume nchini.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma wakati wa kikao kazi kilichoandaliwa na Policy Forum kwa kushirikiana na World Vision, kilichowakutanisha wadau wanaotekeleza afua za haki na ulinzi wa watoto pamoja na Kamati mbalimbali za Kudumu za Bunge.

Katika kikao hicho, TGNP ilishiriki kama mwanachama wa Policy Forum na kuwasilisha uchambuzi kuhusu umuhimu wa bajeti yenye mrengo wa kijinsia katika utekelezaji wa afua za ulinzi wa mtoto ndani na nje ya shule.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC) na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Devota Minja alisema wabunge wako tayari kusukuma ajenda ya ulinzi wa mtoto kupitia mijadala ya bajeti bungeni.

“Sisi kama wabunge kutoka kamati hizi muhimu, tutaenda kusukuma bajeti ndani ya Bunge ili kuhakikisha afua za haki na ulinzi wa watoto zinapatiwa fedha za kutosha,” alisema Devota Minja.



Kikao hicho kilihusisha Kamati za LAAC, PAC, Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati ya Bajeti, huku makatibu wa Bunge na watumishi wengine wa Bunge wakkishiriki katika majadiliano hayo.

Wadau hao walieleza kuwa utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA I) ulikegemea kwa kiasi kikubwa fedha za wafadhili wa nje, ambapo takribani asilimia 85 ya bajeti yake ilitokana na misaada ya wadau wa maendeleo.

Aidha, taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zilibainisha kuwa MTAKUWWA I ilitengewa bajeti kwa asilimia 20 pekee, huku wizara tano tu zikionekana kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo.

Kwa mujibu wa uchambuzi uliowasilishwa, baadhi ya halmashauri zilitenga fedha kwa ajili ya afua za ulinzi wa mtoto lakini fedha hizo hazikutolewa kwa kiwango kilichopangwa. Mfano uliotolewa ni Halmashauri ya Njombe  ambayo ilitajwa kuwa miongoni mwa halmashauri zilizofanya vizuri katika utekelezaji wa bajeti hiyo.

Katika mjadala huo, wabunge walisisitiza umuhimu wa wizara zote kuingiza afua za ulinzi wa mtoto katika mipango na bajeti zao kila mwaka.

Aeshi Hilali ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa PAC alisema ni wajibu wa wabunge kuhakikisha wizara zinatekeleza afua hizo kwa vitendo kupitia bajeti.



“Tuzidai wizara zote zibebe suala la ulinzi wa mtoto katika bajeti zao ili afua hizi zitekelezwe kwa nguvu zote,” alisema Aeshi Hilali.

Naye Mbunge wa Moshi Vijijini, Morris Makoi alisema ulinzi wa mtoto ni suala la kisheria na linapaswa kupewa uzito mkubwa katika usimamizi wa Serikali na Bunge.

Kutokana na majadiliano hayo, wadau walipendekeza Serikali kuongeza uwekezaji kutoka katika mapato ya ndani, kuanzisha mafungu maalum ya kibajeti kwa ajili ya ulinzi wa mtoto, pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha katika ngazi zote za Serikali na halmashauri.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3