PROF MKENDA:MAONI YA WADAU MABORESHO YA SHERIA YA ELIMU KUWASILISHWA BARAZA LA MAWAZIRI
Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda amesema maoni yatakayokusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu maboresho ya Sheria ya Elimu yatawasilishwa katika Baraza la Mawaziri kwa hatua zaidi za maamuzi huku serikali ikilenga kuhakikisha mchakato huo unakamilika ifikapo mwaka 2027.
Prof Mkenda ameyasema hayo jijini hapa wakati akizungumza katika kikao cha kuwasilisha kwa wadau taarifa ya awali ya Kamati ya Mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353.
Amesema serikali imeendelea kufanya maboresho mbalimbali katika sekta ya elimu ikiwemo sera, mitaala, idadi na ubora wa walimu, miundombinu pamoja na vitendea kazi kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu nchini.
Amesema tayari sera mpya ya elimu imezinduliwa na hatua inayofuata ni kufanya maboresho ya sheria ili kuendana na mwelekeo huo mpya wa elimu.
“Tunakutana kwa ajili ya kupitia mapendekezo ya sheria ambayo tayari yamefanyiwa kazi Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 imefanyiwa marekebisho kadhaa, lakini sasa tunakusanya maoni yatakayosaidia kuamua kama tuje na sheria mpya au tufanye maboresho zaidi,” amesema Prof Mkenda.
Aidha, amewashukuru wadau wa sekta ya elimu kwa ushiriki wao katika kutoa maoni na mchango wao unaolenga kuboresha mfumo wa elimu nchini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Caroline Nombo alisema wizara imejipanga kuyachakata na kuyafanyia kazi maoni yote yatakayowasilishwa na wadau.
Amewataka washiriki kuwa wazi katika kutoa maoni yao ili kusaidia kupatikana kwa sheria bora na yenye manufaa kwa taifa.
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir amesema mchakato huo umechukua muda mrefu kwa lengo la kuhakikisha inapatikana sheria inayozingatia maoni ya wananchi wengi na wadau wa elimu.
Mwisho
.jpeg)


.jpeg)

