Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
PPAA YAIMARISHA MFUMO WA RUFAA ZA ZABUNI KWA NJIA YA KIDIJITALI

PPAA YAIMARISHA MFUMO WA RUFAA ZA ZABUNI KWA NJIA YA KIDIJITALI


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

KATIKA hatua inayotajwa kuwa miongoni mwa mageuzi makubwa ya kidijitali kwenye sekta ya ununuzi wa umma nchini, Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) sasa imehamishia rasmi mfumo wa kushughulikia malalamiko na rufaa za zabuni kwenye mfumo wa kielektroniki wa NeST, hatua inayolenga kuongeza uwazi, kupunguza gharama na kurahisisha huduma kwa wazabuni.

Akizungumza jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando amesema mfumo huo umebadili kwa kiasi kikubwa namna taasisi za umma zinavyopokea na kushughulikia malalamiko ya wazabuni, huku ukiwawezesha kufuatilia mwenendo wa rufaa zao moja kwa moja mtandaoni.

Amesema maboresho hayo yametokana na Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za mwaka 2025 ambazo sasa zinahitaji malalamiko yote kuwasilishwa kidijitali kupitia NeST.

Kwa mujibu wa Sando, mfumo huo umetengenezwa kwa ushirikiano kati ya PPAA na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na umeanza kufanya kazi tangu Februari 2025.

Mbali na kurahisisha upatikanaji wa huduma, PPAA pia imeendelea kutoa mafunzo kwa wazabuni, watumishi wa umma na vijana katika maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza uelewa kuhusu haki na fursa zilizopo kwenye zabuni za Serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amepongeza hatua hiyo akisema matumizi ya mifumo ya kidijitali yataongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo na kuimarisha uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.




 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3