M/KITI MAKETE DC AGAWA VIFAA VYA TEHAMA SHULE YA MSINGI MAKETE
Diwani wa Kata ya Iwawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Makete Mfamasia Rabson Mahenge kwa kushirikiana na Wadau waliosoma Shule ya Msingi Makete wamekabidhi vifaa vya Tehama ambavyo ni pamoja na Kompyuta mpakato ( PC ), Kichapishi ( Printer) na Mabunda ya Karatasi ( Ream ) katika Shule ya Msingi Makete iliyopo Kata ya Iwawa wilayani Makete mkoani Njombe ikiwa ni muendelezo wa Kuhakikisha Shule zilizopo Kata ya Iwawa zinafanya vizuri kwenye Taaluma.
Mhe. Mahenge amewataka Walimu kutunza vyema vifaa hivyo vya Tehama ili viweze kufanya kazi kwa muda mrefu na kuwa chachu ya kuongeza kasi ya utendaji kazi wa Shule hiyo.
" Vifaa hivi sio nguvu yangu binafsi bali ni ushirikiano mkubwa ninaopata kutoka kwa Watoto wenu na Wadau mbalimbali waliosoma kwenye shule hii " amesema Mfamasia Mahenge
Pia amewashukuru Wadau na Wazawa wa Makete waliounga mkono mchakato wa kununua Vifaa hivyo ili kuendelea kutengeneza Mazingira mazuri ya Ufundishaji Kwa Walimu wa Shule hiyo.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makete Mwl. Flowin C. Mhapa amemshukuru Diwani huyo kwa kuwakabidhi Vifaa vya Tehama, Pia ameahidi kuleta matokeo Mazuri kwa Mitihani ya Darasa la Saba na Darasa la nne kwani wameboreshewa mazingira ya ufanyaji kazi hususani Kuchapisha Mitihani na Majaribio ambayo ndio nguzo muhimu ya kukuza Uelewa na Kumbukumbu za wanafunzi shuleni hapo.
Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya Shule Ndugu. Anipenda Sanga amewashukuru sana Wadau ambao hawakusita kuunga mkono jitihada za Diwani wa Kata hiyo Mhe. Mahenge kuhakikisha wanatatua Changamoto ya Tehama kwenye shule hiyo.
Pia amewataka Walimu kuendelea kuwa na subira kwa baadhi ya kero ambazo bado hazijatatuliwa kwani ana imani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuzifanyia kazi ili kujenga mazingira mazuri ya ufanyaji kazi wa Walimu hao.
Elllymathew Kika ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo amemuomba Diwani Mhe. Mahenge kuendelea kudumisha umoja na mshikamano baina ya Watumishi wa Serikali na Wananchi wa Kata ya Iwawa kwani ndio chachu matokeo chanya na maendeleo kwenye sekta zote.
Pia amempongeza Diwani kwa jitihada anazozifanya kwenye shule hiyo kuhakikisha Walimu wanapata Mazingira bora ya ufanyaji kazi na Hata kutoa Matokeo mazuri kwenye Mitihani yao ya kujipima kwa ngazi ya Wilaya, Mkoa na hata Taifa kwa Ujumla.



