Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MANISPAA SINGIDA KUCHANJA POLIO II WATOTO 82,000

MANISPAA SINGIDA KUCHANJA POLIO II WATOTO 82,000


Singida.

‎Manispaa ya Singida inatarajia kutekeleza kampeni ya chanjo ya pili, ya ugonjwa wa polio kuanzia Mei 7 hadi 10, 2026, ikiwa na lengo la kuwafikia watoto 82,000 wenye umri chini ya miaka 10, ili kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa huo.

‎‎Kampeni hiyo inakuja baada ya awamu ya kwanza iliyofanyika Machi 24 hadi 27, 2026, iliyohusisha jumla ya watoto 72,000 kuchanjwa, huku hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha watoto wote wanakamilisha dozi muhimu ya chanjo, ili kujikinga na madhara ya ugonjwa wa kupooza.


‎Katika ufunguzi wa mafunzo ya siku moja kwa wahamasishaji, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Singida, Dkt. Godfrey Andrew, alisema mwitikio uliojitokeza katika awamu ya kwanza, unatoa matumaini ya mafanikio zaidi kwa awamu ya pili kufanikiwa, kutokana na juhudi kubwa za uhamasishaji zinazofanywa na timu husika.

‎‎Mafunzo hayo yaliyofanyika ukumbi wa hospitali ya Manispaa ya Singida, yamewakutanisha washiriki kutoka halmashauri ya manispaa na wilaya ya Singida, wakiwemo viongozi wa dini, wazee wa kimila, watu maarufu, viongozi wa serikali za mitaa na wataalamu wa afya, kwa lengo la kuhamasisha jamii kujitokeza, ili kushiriki chanjo hiyo.



‎Kwa upande wake, Magdalena Dinawi kutoka Wizara ya Afya alisema, zoezi hilo ni muhimu kwa watoto waliopata chanjo ya awamu ya kwanza, kuhakikisha wanapatiwa pia awamu ya pili, ili kukamilisha kinga, na amesisitiza kuwa bila kufanya hivyo, juhudi za awali zitakuwa kazi bure.

‎Mratibu wa Chanjo Manispaa ya Singida, Madona Isack, amewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanachanjwa, huku akibainisha kuwa huduma zitatolewa katika maeneo mbalimbali ikiwemo majumbani, shuleni, vituo vya kutolea huduma za afya, na nyumba za ibada.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3