Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 JMAT: TANZANIA HAINA UBAGUZI WA KIDINI

JMAT: TANZANIA HAINA UBAGUZI WA KIDINI

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

KATIBU wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Askofu Israel Maasa, amesema kwa zaidi ya nusu karne Watanzania wa dini zote wamekuwa wakiishi kwa upendo, mshikamano na kuheshimiana bila kujali tofauti zao za kiimani.

Askofu Maasa amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani, umoja na uhuru wa kuabudu kwa dini zote bila ubaguzi wowote, hali iliyosaidia kudumisha mshikamano wa kitaifa kwa miaka mingi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, alisema jumuiya hiyo imesikitishwa na taarifa zilizotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania zinazodai kuwepo kwa ubaguzi wa kidini nchini.

Alisema taarifa hizo, ambazo zinadaiwa kuungwa mkono na baadhi ya wabunge pamoja na Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Marekani, haziakisi hali halisi ya Tanzania na zimewasikitisha pamoja na kuwafedhehesha wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JMAT, Alihadi Mussa Salum, amesema hakuna kundi lolote nchini linalonyimwa uhuru wa kuabudu au kuumizwa kwa misingi ya dini, dhehebu au imani.

Alihadi amesema Tanzania imejengwa katika misingi ya umoja, amani na mshikamano wa kitaifa, hivyo watu wanaoeneza taarifa zinazoipa nchi taswira ya ubaguzi wa kidini wanapaswa kuacha kufanya hivyo.

Aidha, JMAT imeiomba Serikali chini ya Samia Suluhu Hassan kufanya mapitio ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani ili kuonyesha msimamo dhidi ya vitendo vya uchonganishi wa kidini vinavyoweza kuhatarisha amani ya taifa. 

Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3