BUWASA,YASISITIZA USHIRIKIANO WA WANANCHI KULINDA MIUNDOMBINU YA MAJI.
Na Matukio Daima Media
Wadau mbalimbali wa Mtaa wa Kagondo Karuguru Katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wamekubaliana kuanzisha ulinzi shirikishi kufuatia kuongezeka kwa matukio ya wizi wa dira za maji yaliyoripotiwa hivi karibuni katika eneo hilo.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao kilichoandaliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo kwa lengo la kujadili namna ya kutokomeza vitendo vya wizi wa dira za maji vinavyoendelea kuwasumbua wakazi hao.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa BUWASA, Bi Julieth Shangali, amesema mamlaka hiyo imepokea kwa uzito mkubwa taarifa za wimbi la wizi wa dira za maji katika Kata ya Kagondo na kuamua kuitikia wito wa wananchi kwa kufanya kikao hicho cha pamoja kutafuta suluhisho la tatizo Hilo.
Amesema BUWASA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inaendelea na uchunguzi wa kuwabaini wahusika wa vitendo hivyo, ambapo tayari dira mbili kati ya 12 zilizoibwa zimepatikana huku msako ukiendelea.
“Tumekuja kujadiliana nanyi hapa ili kuona namna bora ya kukomesha wizi huu kama ilivyofanikiwa katika maeneo mengine. Ushirikiano wenu kama wananchi ni muhimu ili kulinda miundombinu hii muhimu,” amesema Bi Shangali.
Aidha, wananchi walishauriwa kujengea sehemu za dira zao za maji ili kupunguza uwezekano wa kuiba dira ili kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kupatikana bila usumbufu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja , Bi Devotha Koy, amewataka wananchi kuwa walinzi wa kwanza wa dira zao kwa kuwa mteja atalazimika kugharamia dira mpya endapo itaibiwa.
“Ni muhimu kila mwananchi kuhakikisha analinda dira yake kwa sababu ikipotea atalazimika kulipia nyingine ili kuendelea kupata huduma ya maji,” amesema Bi Koy.
Katika hatua nyingine, wadau wa kikao hicho walikubaliana kuanza rasmi mpango wa ulinzi shirikishi katika mtaa huo, huku BUWASA ikiahidi kutoa baadhi ya vifaa vya kusaidia utekelezaji wa zoezi hilo ikiwemo tochi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Bukoba, viongozi wa mtaa pamoja na wananchi wa Kagondo Karuguru.





