REA YABAINISHA VIPAUMBELE WATAKAVYOANZA NAVYO KWA MWAKA WA FEDHA 2026/2027
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
MWANZA, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imebainisha vipaumbele vya msingi watakavyoanza navyo kwa mwaka ujao wa fedha wa 2026/2027 ili kuhakikisha kwamba miradi ya nishati inatekelezwa kwa ufanisi zaidi katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza katika Mkutano katika wa kwanza wa mwaka uliowakutanisha Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wadau wa Maendelo Jijini Mwanza, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Said, amevitaja vipaumbele hivyo vitahusisha kuharakisha uunganishaji wa umeme kwa wananchi, kuongezeka kwa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, kuboresha matumizi ya umeme kwa shughuli za maendeleo, kuimarisha miundombinu ya grid ndogo za kuzalisha umeme wa jua, pamoja na mifumo mingine ya nishati mbadala.
Amefafanua kuwa mwaka wa fedha, REA imetenga sehemu kubwa ya bajeti yake kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya usambazaji umeme na kuharakisha uunganishaji wa umeme katika maeneo ya vijijini mikakati mkakati huo ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha kuwa huduma ya umeme inafikia maeneo yote, na kusaidia katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Tutahakikisha kuwa watumishi wetu wanapata mafunzo ya kutosha, ili waweze kutoa huduma bora na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini,” Alisema Saidy.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alisisitiza kuwa vipaumbele vya REA vitakuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hasa katika vijijini.
Mtanda alisema kuwa, katika mkoa wa Mwanza, REA imeweza kutekeleza miradi kadhaa ya nishati, ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme katika vijiji, usambazaji wa majiko banifu, na miradi ya umeme wa jua na aliongeza kuwa serikali kupitia REA imewekeza zaidi ya shilingi milioni 127.7 kwa ajili ya miradi ya nishati katika mkoa wa Mwanza.
"Hii ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha kuwa wananchi wetu wanapata huduma ya umeme, na kwamba tunatoa suluhu endelevu kwa changamoto za nishati vijijini," Alisema Mtanda.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini REA, Balozi Meja Jenerali Jacob Kingu, ameeleza kuwa Wabia wa Maendeleo Wana Mchango Mkubwa katika kutekeleza miradi ya nishati na kufafanua kuwa ili kufanikisha miradi ya nishati safi ya kupikia na umeme wa jua, wabia wanahitaji kutoa msaada wa kifedha na kushirikiana na REA kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa ufanisi.
Kingu alibainisha kuwa wabia wa maendeleo wanahitaji kuona matokeo ya fedha wanazotoa kwa kuhakikisha kuwa miradi ya nishati inasaidi jamii na kuhamasisha uchumi wa vijijini.
"Nishati ya umeme na nishati safi ya kupikia ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na wabia wa maendeleo wanahitaji kuhakikisha kuwa wanatoa msaada wa kifedha ili miradi hii iweze kufanikisha malengo yake," alisema Kingu.
Mhandisi Said alisisitiza kuwa mpango huu unalenga kutoa umeme katika maeneo ya vijijini, hasa maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma ya umeme.







