WILAYA YA LINDI KUPANDA MITI LAKI MBILI KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA MISITU DUNIANI
Na Hadija Omary ,Matukio Daima ,Lindi
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani pamoja na Juma la Upandaji wa Miti Kitaifa, Manispaa ya Lindi inatarajia kupanda jumla ya miti laki mbili katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira na kuimarisha uchumi endelevu.
Uzinduzi wa zoezi hilo umefanyika katika Shule ya Msingi Msinjahili iliyopo Manispaa ya Lindi, ambapo miti ya matunda, miti ya mbao pamoja na miti ya kivuli imepandwa na wadau mbalimbali wa mazingira.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bi. Victoria Mwanziva, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa wingi na kuitunza ili kuenzi kaulimbiu ya maadhimisho hayo isemayo “Misitu ni Uchumi Endelevu, Tuhifadhi kwa Maendeleo ya Taifa.”
Kwa upande wake, Afisa Misitu Mkuu kutoka Idara ya Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Simon Kiteleja, amesema zoezi hilo ni mwendelezo wa kampeni ya upandaji miti kitaifa kuelekea Siku ya Misitu Duniani. Amesema maadhimisho ya mwaka huu yanatarajiwa kufanyika kitaifa katika Mkoa wa Lindi ambapo Manispaa ya Lindi itakuwa mwenyeji.
Naye Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Lindi, Gaspar Vicente, amesema katika Shule ya Msingi Msinjahili wanatarajia kupanda miche 1,500 ikijumuisha miti ya matunda, mbao na kivuli. Ameeleza kuwa mkakati wa TFS ni kuzalisha miche laki mbili kila mwaka ili kuendelea kuhamasisha upandaji miti na uhifadhi wa mazingira.
Uongozi wa Shule ya Msingi Msinjahili umeahidi kushirikiana na wanafunzi pamoja na jamii inayozunguka shule hiyo katika kuitunza na kuilinda miche iliyopandwa ili iweze kukua na kutoa manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho



