Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WAZIRI DKT GWAJIMA AFUATILIA SAKATA LA BINTI WA MIAKA 12 KUDAIWA KUOZESHWA UVINZA

WAZIRI DKT GWAJIMA AFUATILIA SAKATA LA BINTI WA MIAKA 12 KUDAIWA KUOZESHWA UVINZA

TAZAMA VIDEO BOFYA HAPA

Na Matukio Daima Media 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, amesema anafuatilia kwa karibu taarifa za sakata la binti mwenye umri wa miaka 12 anayodaiwa kuozeshwa kwa nguvu na baba yake katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Kwa mujibu wa taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, tukio hilo linadaiwa kutokea katika Kijiji cha Kisirisiri, Kata ya Mjabibi, wilayani humo, ambapo binti huyo anayeitwa Neema anadaiwa kuozeshwa na baba yake mzazi, Nashon Lucas.

Akitoa maoni yake kupitia ukurasa wa Instagram wa Matukio Daima Habari, Waziri Dkt Doroth Gwajima amesema tayari ameanza kufuatilia suala hilo kwa kuwasiliana na viongozi wa mkoa na wilaya husika.

“Hongereni kwa kazi njema. Ngoja nami nimtafute Mheshimiwa DC Uvinza na RC Kigoma na Ofisi ya Waziri wa Nchi, TAMISEMI,” aliandika Waziri Gwajima katika maoni yake.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mwandishi wa habari Zulfa Mfinanga, inadaiwa kuwa binti huyo alifiwa na mama yake tangu akiwa mdogo na tangu wakati huo amekuwa akiishi chini ya uangalizi wa baba yake.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa miaka miwili iliyopita baba huyo alijaribu kumuozesha pia dada yake Neema, lakini binti huyo alifanikiwa kutoroka na kwenda kuishi kwa bibi yake mzaa mama. Hata hivyo, baba huyo anadaiwa kufika nyumbani kwa bibi huyo na kuchoma moto nyumba yake.

Inadaiwa kuwa binti huyo mkubwa aliondoka kabisa katika kijiji hicho na hajawahi kurejea tena hadi sasa.

Aidha, taarifa hizo zinaeleza kuwa wiki iliyopita baba huyo alimuoza Neema kwa mwanaume ambaye tayari ana wake wawili, hivyo kumfanya mtoto huyo kuwa mke wa tatu.

Kinachozua huzuni zaidi katika tukio hilo ni kwamba inadaiwa binti huyo hajawahi kupelekwa shule tangu kuzaliwa kwake.

Wananchi na wadau wa ustawi wa watoto wameomba mamlaka husika katika Wilaya ya Uvinza  na Mkoa wa Kigoma  kuchukua hatua za haraka kuchunguza tukio hilo na kuhakikisha mtoto huyo analindwa pamoja na haki zake kulindwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Juhudi za kuwatafuta viongozi wa wilaya na mkoa huo ili kuzungumzia tukio hilo zinaendelea huku wananchi wakisubiri hatua za mamlaka kuchukuliwa.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3