WANAWAKE LINDI WAHAMASISHWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UCHIMBAJI MADINI
NA HADIJA OMARY ,MATUKIO DAIMA MEDIA ,LINDI
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, ametoa wito kwa wanawake wa mkoa huo kujisimamia kiuchumi kwa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana katika maeneo yao, hususani katika sekta ya uchimbaji wa madini.
Telack ametoa wito huo wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika katika kijiji cha Mbekenyera, wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Telack amesema kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kujitegemea kiuchumi bila kusubiri kuwezeshwa, endapo wataamua kutumia vyema fursa zilizopo katika maeneo yao.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuwawezesha wanawake kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake, Naomi Festo, mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya Kinywe Lindi Jumbo, amesema umefika wakati kwa wanawake kuchangamkia fursa katika sekta ya madini ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikionekana kuwa ni shughuli za wanaume pekee.
Amesema ushiriki wao katika maonesho yaliyofanyika katika maadhimisho hayo unalenga kuwakumbusha na kuwahamasisha wanawake kuona umuhimu wa kuingia katika sekta ya madini na kunufaika na fursa zilizopo.
Naye Kaziana Robert kutoka kampuni ya MSALABS amesema sekta ya madini imekuwa ikitoa fursa mbalimbali kwa watu bila kujali jinsia, hivyo ni muhimu wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za sekta hiyo.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hufanyika kila mwaka tarehe 8 Machi, yakilenga kuhamasisha usawa wa kijinsia pamoja na kuwainua wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
.jpg)

