Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TAFITI ZA BIASHARA NA VIWANDA KUIMARISHA TAKWIMU ZA MAENDELEO NCHINI

TAFITI ZA BIASHARA NA VIWANDA KUIMARISHA TAKWIMU ZA MAENDELEO NCHINI

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

SERIKALI kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeanza utekelezaji wa tafiti mbalimbali zenye lengo la kukusanya taarifa muhimu kuhusu shughuli za biashara katika sekta rasmi na isiyo rasmi pamoja na uzalishaji viwandani nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dkt. Amina Msengwa amesema tafiti hizo zinalenga kupata takwimu sahihi kuhusu uzalishaji, ajira, uwekezaji na mazingira ya biashara ili kubaini mwenendo wa ukuaji wa biashara na viwanda nchini.

“Tafiti hizi zina lengo la kukusanya taarifa muhimu kuhusu shughuli za biashara katika sekta rasmi na isiyo rasmi ikiwemo uzalishaji viwandani, ajira, uwekezaji na mazingira ya biashara ili kubaini mwenendo wa ukuaji wa biashara na viwanda nchini,” amesema Dkt. Msengwa.

Amesema taarifa zitakazokusanywa zitaisaidia Serikali pamoja na wadau wa sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na watafiti kubuni programu na mikakati ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Aidha, utafiti wa Huduma za Fedha kwa Wafanyabiashara (Finscope MSME) utatoa takwimu muhimu kuhusu upatikanaji wa mikopo, akiba, bima na huduma za fedha za kidijitali kwa biashara ndogo sana, ndogo na za kati.

“Taarifa zitakazopatikana zitatumika kupima maendeleo ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Ujumuishaji wa Kifedha Awamu ya Tatu pamoja na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha,” amesema.

Kwa mujibu wa Dkt. Msengwa, pia kutafanyika utafiti wa uzalishaji viwandani utakaokusanya taarifa kuhusu orodha ya viwanda katika mikoa mbalimbali, aina ya bidhaa zinazozalishwa, idadi ya wafanyakazi, gharama za uzalishaji na mapato ya viwanda.

“Taarifa nyingine zitakazokusanywa ni pamoja na masoko, teknolojia ya mitambo, usimamizi wa mazingira, mipango ya uwekezaji na changamoto zinazovikabili viwanda nchini,” amesema.

Tafiti hizo zitafanyika katika maeneo 1518 ya utafiti nchini ambapo biashara na taasisi 8,624 pamoja na viwanda 4,245 vinatarajiwa kushiriki katika zoezi hilo.

Serikali imewataka wananchi watakaofikiwa na wadadisi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu bora zitakazosaidia kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya taifa.

Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3