MEDIA BRAINS YAWANOA WAANDISHI ARUSHA, YATOA MBINU KUPAMBANA NA HABARI ZA UONGO
.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kihabari ya Media Brains Jesse KwayuNa ZULFA MFINANGA,
MATUKIO DAIMA, ARUSHA.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kihabari ya Media Brains, Jesse Kwayu, amesema kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia kwa kujifunza mbinu mpya za uandishi wa habari za mtandaoni ili kuendelea kutoa taarifa sahihi na zenye tija kwa jamii.
.Kwayu ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na kampuni hiyo kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Arusha, yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kuandika na kuripoti habari za mtandaoni katika mazingira ya sasa ya maendeleo ya teknolojia.
Ameeleza kuwa kwa sasa tasnia ya habari imebadilika kwa kiasi kikubwa na kuhamia zaidi kwenye majukwaa ya mtandaoni, hali inayohitaji waandishi wa habari kujifunza mbinu mpya za uandishi pamoja na matumizi sahihi ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya akili unde (AI) katika ukusanyaji na uchakataji wa taarifa.
Mbali na hilo, amesema mafunzo hayo pia yamelenga kuwasaidia waandishi wa habari kutambua na kuchambua taarifa za uongo na uzushi ambazo zimekuwa zikisambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya kidijitali
Baadhi ya washiriki wamesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kutokana na kuongezeka kwa taarifa zisizo sahihi katika jamii, hali inayotokana na kukua kwa teknolojia na urahisi wa kusambaza habari kupitia mitandao ya kijamii.
“Bila kuwa na maarifa ya kitaaluma ni ngumu kujua taarifa husika ni ya kweli au ya uongo, lakini mafunzo haya yametoa elimu kwa waandishi kutumia zana za kiteknolojia za kupima na kubaini habari sahihi na zile za uongo,” amesema Ashura Mohamed, mwandishi wa habari kutoka Radio 5.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Claud Gwandu, amesema waandishi waliopata mafunzo hayo wanatarajiwa kuwa mfano kwa wengine kwa kuhakikisha wanazingatia maadili ya taaluma na kuepuka kusambaza habari zisizo na uthibitisho katika majukwaa ya mtandaoni.



