Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
JUMUIYA YA ISTIQAAMA KWA KUSHIRIKIANA NA GBP TANZANIA WATOA MSAADA SHIRIKA LA (SOS).

JUMUIYA YA ISTIQAAMA KWA KUSHIRIKIANA NA GBP TANZANIA WATOA MSAADA SHIRIKA LA (SOS).

 

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

MWANZA, Jumuiya ya Istiqaama tawi la Mwanza kwa kushirikiana na GBP Tanzania wametoa msaada wa vyakula kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha  Children’s Village Tanzania (SOS) Mkoani Mwanza, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea sikukuu ya Eid el-Fitr kwa waumini wa dini ya Kiislamu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Sheikh Nuhu Mousa kutoka Jumuiya ya Istiqaama tawi la Mwanza ameeleza kuwa kitendo hicho ni sehemu ya kuwakumbuka watoto yatima na kurejesha furaha katika mioyo yao.

Mousa ameleza kuwa Eid al-Fitr ni sikukuu yenye umuhimu mkubwa, na hakuna jambo la thamani kama kuwafariji watoto waliokosa malezi kwa kuwapa matumaini na furaha.

“Watoto yatima ni kundi muhimu katika jamii, na Mtume amesisitiza sana kuwalea na kuwajali. Kwa niaba ya Jumuiya ya Istiqaama, tumekuwa tukifanya zoezi hili kila mwaka ili kuwarudishia furaha watoto hawa,” alisema Sheikh Osman.


Kwa upande wake, mwakilishi kutoka GBP Tanzania, Seif Rashidi, alisema kuwa kuwakumbuka watoto yatima ni jambo la heri na rehema linalohitaji moyo wa kujitolea.

Aidha alibainisha kuwa si kila mtu anaweza kuwa na moya wa kujiyolea kuhakikisha wanawajali watoto hao, lakini pia jamii ina wajibu wa kuhakikisha watoto hao wanapata malezi na furaha wanayostahili.

“Ni mtihani ambao umewapata watoto hawa, lakini pia unaweza kutupata sisi. Hivyo ni wajibu wetu kama jamii kuwasaidia, kwani hawa ndio kizazi kijacho kitakacholijenga taifa,” alisema Rashidi.

Naye mwakilishi wa SOS Children’s Village Tanzania, Victor Wilson, aliwashukuru wadau hao kwa kuendelea kuwasaidia watoto walioko katika mazingira magumu, akisema msaada huo umekuwa baraka kubwa kwao.

Wilson ameeleza kuwa watoto wengi waliopo katika kituo hicho walifika wakiwa hawana msaada wala malezi, hivyo michango ya wadau imekuwa msaada mkubwa katika kugharamia mahitaji yao muhimu kama chakula, elimu na malazi.

“Msaada huu unawafariji watoto na kuwasaidia kutimiza ndoto zao. Tunawashukuru sana GBP Tanzania kwa kuendelea kutukumbuka kila mwaka,” alisema Wilson.

Kwa upande wake, mama mlezi katika kituo hicho, Shela Mohamed, alisema msaada huo umeleta furaha kubwa kwa watoto, kwani unawafanya wajisikie kuthaminiwa na kujua kuwa kuna watu wanawajali.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3